Wednesday, 26 February 2014
SOMO: KIONGOZI BORA WA KIROHO [KIKRISTO]
MWL: MWINJ & MCH. SONGWA .MM. KAZI.
SIMU: 0757 – 567899/ 0789 – 567899/ 0719 – 968160/ 0779 – 597066
TAG – KONGOWE – FOREST P.O. BOX 70983 DAR ES SALAAM.
Email: songwak@yahoo.com. ptrsongwak@gmail.com
YALIYOMO:
Utangulizi.
Maana ya Uongozi.
Maana ya Kiongozi.
Tofauti ya kiongozi wa Kiroho na wa Ki - dunia.
Umuhimu wa Uongozi/Kiongozi.
Sura ya Uongozi/Kiongozi wa kiroho.
Maadili ya Kiongozi wa Kiroho.
Changamoto za Kiongozi/Uongozi.
Mafao (Thawabu), Gharama na Anasa za Uongozi.
Siri ya mafanikio ya Uongozi wa Kiroho.
Kiongozi mwenye maono na malengo na mipango.
Aina mbili ya Kiongozi.
Kiongozi anayefaa kuigwa na watu.
Misingi ya Kiongozi/Uongozi wa Kiroho.
Lugha ya Kiongozi.
Sifa za jumla za Kiongozi wa Kiroho.
Wajibu wa jumla wa Kiongozi wa Kiroho.
01. UTANGULIZI.
Je, Kiongozi anahitajika? Nini umuhimu wakuwa na Kiongozi?
Je, Unajua tofauti kati ya Uongozi na Utawala?
Je, Wewe ni kiongozi au Mtawala?
Popote unapoona kazi ya Mungu imesonga mbele na kufanya vizuri lazima kuna kiongozi aliyesimama kwenye nafasi yake vizuri.
Imekuwa ni tabia ya Mungu mara zote kumchagua mtu ili kuyafanikisha malengo na mipango yake.
Mfano: Mungu alimuandaa Ibrahimu na kumwita ili kuanzisha Taifa - Mwanzo 12: 1-2; Akamwandaa Yusufu ili kulihifadhi Taifa hilo - Mwanzo 45: 3 - 9, 50: 20 - 21. Akamwandaa Musa ili kulitoa Taifa hilo Utumwani - Kut.3:2-14. Akamwandaa Joshua kuliongoza Taifa hilo kuteka nyara, kupigana vita na kuliingiza Kanani - Yoshu 1: 1 - 9. Mungu alitumia wanaume na wanawake katika kufikia malengo yake kama vile Nabii Debora - Amuzi 4:4, Esta 7: 3 - 6 n.k.
Pia Mungu aliwaongoza na kuwaelekeza waamuzi na wafalme katika kulisimamia kundi lake (watu) wa Mungu, pia aliwatumia Manabii ili kuwaonya na kuwasahihisha watu wa Mungu; Na hatimaye alimtuma mwanaye wa pekee mpendwa Yesu Kristo kuja kufa na kufufuka kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu kutoka katika utumwa wa dhambi - Yoh. 3:16, Math. 1:21.
Yesu naye alipoondoka akamtuma Roho Mtakatifu ili atuongoze salama - Yoh. 14: 16,26, Rumi. 8:14
Jambo la pekee katika ufalme wa Mungu, mtu mmoja anaweza akaleta/akasababisha ushindi mkuu katika kanisa au Huduma. Hii ni ajabu Mungu anasema katika Ezek. 22:30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakaye tengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.”
Kumbuka:
Hitaji kubwa la nyakati zote tangu vizazi na vizazi, katika watu wa kada zote, jamaa, Taifa, Mataifa, Taasisi na Mashirika ya dini ni kupata viongozi wenye sifa na uwezo wa kuwaongoza wengine, pia wenye uwezo na hekima katika kuwaunganisha watu ili kuwafanya kuwa wamoja katika kutumia karama, vipawa, talanta, huduma na rasilimali walizonazo kwa manufaa ya maendeleo yao. Pia waweze kufikia na kukamilisha jambo/malengo na mipango yao waliyokusudia.
Viongozi wanajua wanalopaswa kulifanya na wana uwezo wa kuwachukua watu mbele zaidi ya pale walipo sasa.
*MAANDIKO YA SOMO LA MSINGI*
Marko.10:45, 1Petr.2:21, Yoh.10:10 - 11
02. MAANA YA UONGOZI.
Uongozi ni hali/tendo la kuongoza.
Ni hali ya kutangulia mbele, kusimamia, kulinda na kuelekeza watu njia au mwelekeo wa kuuendea au kufikia malengo Fulani.
03. MAANA YA KIONGOZI: Mark.10:45, 1Tim.4;11 - 12, 1Petr.2:21.
Kiongozi ni mtu Yule ajuaye njia na yale apaswayo kupita nayo na kuzingatia katika njia hiyo.
Ni mtu Yule ajuaye mwelekeo wa jambo hilo au malengo hayo na anauwezo wa kuwatangulia na kuwavutia (shawishi) wengine wamfuate.
Ni mtu aliyepewa dhamana (aliyeaminiwa) na Mungu kuongoza watu wengine (kuwatumikia). Mfano: Yesu - Yoh.14:6; 10:2 - 4, Paulo - 1Kor.11:1; 4:16.
Ni mtumishi (mtumwa) wa wale anaowaongoza.
Mfano: Musa - Kut.10:25 - 26; 13:21 - 22, Yuda - Mw.46:28
Kumbuka:
Kiongozi wa Kiroho siyo mtawala (boss) bali ni mtumishi (mtumwa).
Kiongozi ni kielelezo (mfano) wa kupigiwa, kufuatwa na kuigwa na wengine - Unaosimama mbele yao kuwaongoza.
Hivyo maisha ya kiongozi lazima yawe kielelezo katika maeneo matano (5) yafuatayo:-
Katika Usemi: Chunga (angalia) sana matumizi ya ulimi (yale uyasemayo).
Yakobo 3:1 - 12.
Katika Mwenendo: (Tabia) - Maisha yako ya kila siku machoni pa watu.
Math.5:16, 1Petr.2:11 - 12, Fil.2:14- 16.
Katika Upendo: Kujitoa, kujali, kuhudumia na kuhurumia. Yoh.3:16,
Math.9:35 - 38.
Katika Imani: Maisha ya kumtegemea Mungu. Ebr.10:38; 11:1,6,
Hesabu.14:11, Yer.17:5 - 8, Rumi.1:17, Gal3:11.
Katika Usafi: Maisha Matakatifu - yenye ushuhuda mzuri mbele za watu.
Zb.16:3, Kumb.23:14, 1Kor.3:16 - 17, 1Petr.1:16.
04. TOFAUTI YA UONGOZI/KIONGOZI WA KIROHO NA WA KIDUNIA.
Uongozi wa Kiroho na ule wa kidunia unaweza ukafanana katika baadhi ya mambo Fulani tu, lakini ukatofautiana sana na kwa kiasi kikubwa katika mambo ya kimsingi.
Kwa mfano katika mambo yafuatayo:-
i) Hitaji na namna ya kumuandaa Kiongozi.
Mungu huandaa na kumweka Kiongozi. 1Sam.16:3,7 Ezek.16:1 - 5, 1Tim.3:1,15 Yer.3:15 Math.9:38.
ii) Nia ya ndani ya Kiongozi.
Swali la kimsingi la kujiuliza, Kwanini wewe ni Kiongozi? au kwanini unataka kuwa Kiongozi?
Zipo nia mbalimbali kama vile kutaka:- mamlaka, sifa, kuheshimiwa, utukufu, kutambulika, kiburi n.k.
*Hizo ni nia za Kiongozi wa Kidunia*
Pia mtu anaweza kuwa kiongozi kwa nia ya kutaka kuyafanya mapenzi ya Mungu. FIlipi.2:5, 13.
Kumbuka:
Uongozi wa kidunia unadhihirishwa katika nia binafsi katika kupata mafao yenye kumnufaisha yeye na familia yake, kupata marupurupu mazuri, heshima; bila kujali wengine kama wanaumia au la, hivyo watu wanapigania kuwa viongozi katika kutoa rushwa kwa nia ya cheo na siyo huduma itakayotolewa au utendaji.
Uongozi wa Kiroho, Mungu anasema “Msitende neno lolote kwa kushindana wala majivuno, bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Fip.2:3 - 4.
iii) Kutaka mapenzi ya Mungu. Rum.12:2, Efe.5:17, 1Tim.3:1
Nia yake ya moyoni ndiyo itakayobainisha kama atakuwa wa Kiroho au wa Kidunia.
Kumbuka:
Kiongozi wa Kiroho, yeye ni kiungo au mpatanishi kati ya Mungu na watu anaowaongoza.
Mfano: Musa - Kutoka.19:9; 24:3, Yesu - Yoh.8:26 - 30, Paulo - 2Kor.5:18 - 20.
05. UMUHIMU WA UONGOZI/KIONGOZI.
Tumeona uongozi ni muhimu sana mbele za Mungu na kwa watu pia.
Uongozi ni kipawa (zawadi) ya Mungu kwa wanadamu ili wakae katika amani, utulivu na matumaini. Bila uongozi watu hukosa mwelekeo (dira) na amani, hivyo hufikia hatua ya kufarakana, kutawanyika, kukosa mwelekeo, kila mtu kwenda au kutenda lile analoona linamfaa yeye machoni pake. Rejea baada ya Yoshua kushindwa kuandaa kiongozi, pindi alipokufa wana wa Israel walipoteza mwelekeo kabisa, kila mwamuzi aliibuka na mfumo wake kwani hakuwepo kiongozi. Kwa sababu hiyo Mungu ameweka Uongozi ili watu wapate mwelekeo, amani na matumaini katika kuyatimiza mapenzi yake duniani. Tazama Amuzi. 21:25 watu walijiendea hovyo hovyo, Zek. 13:7 - Nitampiga Mchungaji. Hesabu. 27:15 - 23, Efeso. 4:11 - 13.
06. SURA YA UONGOZI/KIONGOZI WA KIROHO.
Yapo mambo mengi ya kuangalia au yanayotakiwa kuonekana ndani ya Uongozi wa Kiroho ila haya matatu ni ya msingi sana kutupa sura ya kiongozi wa kiroho:-
i) SURA YA UTUMISHI:
Mark. 10:45, Lk. 22:24 - 27, Math. 20:24 - 28, Yoh. 13:1 - 17 (mst 14, 17)
Je, wewe ni kiongozi wa aina gani?
Mimi ni Kiongozi ninayeongoza.
Mimi ni Mtumishi ninayetumika.
Mimi ni Kiongozi Mtumishi.
Mimi ni Mtumishi Kiongozi.
Mtumishi Kiongozi:
Hii ni falsafsa (msemo/imani) inayowasaidia watu kuwa na dhana ya utumishi; na baadaye kuweza kuongoza kwa nia ya kuwatumikia watu, shirika, kanisa, n.k.
Mtumishi kiongozi anaweza asiwe na cheo/nafasi yoyote kanisani na bado akawa tegemeo (nguzo) kwa kanisa au watu wengi na kutoka kwake watu wanaweza kupokea hazina njema.
Mchungaji wangu kiongozi Rev. Victor Tawete wa TAG Kongowe Forest siku moja alisema katika fafanuzi yake ya neno mtumishi kuwa “Kipimo cha mtumishi ni kiwango cha mtumishi (mhudumu) wa Hotelini, maarufu kama waiters hata kama akitumwa vipi hakwaziki na wala hakasiriki, akaongeza akisema mtumishi kiongozi ni Yule anayetumiwa na watu wengine kwa kadri wapendavyo wao.”
Neno la Mungu linaonyesha maneno ya msingi na yenye hekima katika utumishi kama ifuatavyo:-
Lk. 22:26 - 27, Math. 20:26 - 28, 1Petr. 5:2 - 3.
Tabia ya Mtumishi Kiongozi.
Mnyenyekevu - Math. 10:24, 2Tim. 2:25, 1Petr. 5:5 - 7.
Ana bidii - Si mvivu - Math. 24:45 - 47.
Ana uwezo wa kufundisha - 2Tim. 2:24.
Mvumilivu - 2Tim. 4:2.
Mtii - Efeso. 6:5 - 6, Tito. 2:9.
Anajitoa - 2Sam. 15:21.
Mwangalifu - 1Sam. 22:14.
Amejaa Roho Mtakatifu - Mdo. 2:16,18.
Anakubali Maonyo - Mhubiri. 4:13.
II) SURA YA UCHUNGAJI:
Zab. 23, Yoh. 10:11; 21:15 - 17, 1Petr. 5:2 - 3.
Kiini cha Uchungaji:
Neno Mchungaji lilitumika sawa na mchungaji wa kondoo, ng’ombe au mifugo mingine. Yer. 6:3, Math. 8:33
Mchungaji hukaa na kondoo na kazi yake muhimu ni kuwa na kondoo hizo.
Kumbuka:
Kondoo ndiyo wanampa kazi ya kuwa mchungaji, hivyo mchungaji ni mtumishi wa kondoo (watu).
Sifa ya Mchungaji:
Anawajua kondoo wake kwa majina - Yoh. 10:3, 14, 27. Sawa na Haruni juu ya wana wa Israel - Kut. 28:9, 10, 12, 29.
Yuko pamoja na kondoo au anapatikana na ni rahisi kuingilika Lk. 22:27.
Anatangulia mbele kuwaonyesha kondoo njia, mahali pa malisho, majani na maji.. Zab. 23:1 - 2.
Ni jasiri na yuko tayari kujitoa kwa ajili ya kondoo. Yoh. 10: 10 - 13.
Anawaongoza na kuwaelekeza kwa upole kwa fimbo ya kichungaji. Zab. 23:4, Ufu. 21:15.
Ili kutimiza wajibu wake kwa kondoo (washirika/kanisa):
Kiongozi wa sura ya mchungaji anapaswa kujua mambo makuu matatu,
nayo ni:-
i) Kwamba ameitwa na Mungu - Yh. 15:16.
ii) Kufahamu chanzo cha nguvu zake - Kol. 1:11, 29. Zek.4:6.
iii) Kufahamu mambo aliyoitiwa kufanya, na hata jinsi ya kuyapatia vipaumbele -
Yoh. 10:4.
Mambo hayo humfanya mchungaji kuwa na maono, malengo na mipango mizuri katika uongozi (kazi), huduma yake. - Kol. 1:10, Efes. 4:1.
Mchungaji anapaswa kuhakikisha kuwa kundi lake:-
Linaongezeka kiidadi - Mdo. 2:47, 41: 6 - 7.
Linakuwa kiroho - Mdo. 2:42, 2Kor. 2:14, Kol. 1:10.
Linamwabudu Mungu katika Roho na kweli - Yoh. 4:24, 2Kor. 4:24, 2Kor. 4:2.
Linahifadhi umoja wa roho na ushirika katika mwili wa Kristo - Fil. 1:27, Efe. 4:1 - 6.
Linashuhudia ulimwengu habari njema na kuwaleta watu kwa Kristo (Uinjilisti) - Mdo. 5:42; 6:7, Math. 20:18 - 20.
Linapata ulinzi, usalama na amani - Mdo. 20:28 – 31
Tahadhari ya Mchungaji (kiongozi) kama kuhani wa Mungu ni kuona kuwa:-
Asiwe sababisho la kundi kutawanyika katika uongozi wake. Yer.23:1 - 2, Ezek.34:2 - 5, 10.
Hapotoshi mafundisho ya kweli ya Mungu; yaani hafundishi kwa nia ya kudanganya kundi kwa manufaa yake binafsi. Ezek. 22:26, 30, Tito. 2:7 - 8, Ezek. 13:1 - 7, Isa. 10:1- 3, Yer. 14:14, Isa. 30:10, Yer. 23:21 - 22, 2thes. 2:9 - 12.
Anatoa malisho kwa kundi kama unavyokusudia na kwa wakati unaokubalika. Yer. 23:22, Math.24:45 - 46, 2Tim. 2:15, 2Tim.4:5.
Kumbuka:
Kwa kuyafanikisha haya mchungaji (kiongozi) lazima azingatie yafuatayo:-
Maombi na (b).Kusoma neno la Mungu na kulitafakari kila wakati. Math. 17:20 - 21, Yoh. 15:7, Fil. 4:16, 1Thes. 5:17, Kol. 3:16, Yoh. 17:14 - 17.
III. SURA YA UWAKILI.
Math. 25:14, 1Kor. 4:1 - 2.
Wakili: Ni mtu yeyote anayepewa uwezo na mtu mwingine ili kusimamia mambo yake.
Wakili: Ni mtu anyemtetea mtu mwingine mahakamani.
Katika Agano jipya wakili ni mtu aliyeaminiwa na bwana wake; na hivyo alipewa mafao na mamlaka na pia alikuwa na wajibu na uwajibikaji kwa kazi yake. Lk. 12:42 - 43.
Wajibu wa Wakili ulikuwa ni:-
Kuangalia vipawa katika maisha ya wale anaowaongoza ili avitumie vizuri na kuzalisha. 2Tim. 1:14, 1Tim. 1:18 - 20.
b) Kuhesabu rasilimali zote alizonazo, kama vile watu, fedha, vifaa na kwa neema ya
Mungu kuweza kupanga na kuvitumia ipasavyo.
c) Kuwa mkweli (honesty) - mwenye msimamo mwema mwadilifu (integrity) na
muwazi (transparency) - Yoh. 8:12.
Kuwa mwaminifu (faithful) na mwenye kupandishwa daraja kwa sababu ya
uaminifu wake. - Math. 25:21, 1Kor.4:1 - 2, Math. 24:45 - 47.
07. MAADILI YA UONGOZI/KIONGOZI WA KIROHO.
Maadili ni tabia njema ya mtu au mwenendo mwema (mzuri) wa mtu.
Tabia - Ni mazoea ya hali Fulani au vitendo fulani.
Maadili ni jambo linaloweza kutenganisha sifa za kiongozi katika mwonekano wake kati ya uongozi wa Kiroho na wale wa kidunia.
Maadili yapo hasa kuonyesha msimamo katika usafi wa maisha na haki.
1Kor. 10:23, 6:12.
Swali la kujiuliza;
Unajisikiaje kwa yale unayoyafanya mbele za Mungu na wanadamu?.
Je, ni sawa au si sawa?
1Tim. 3:2 - 12.
Neno la Mungu linaeleza maadili ya msingi kwa kiongozi wa Kiroho ya kuwa anapaswa awe mtu wa:-
Kutolaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, na busara, mtaratibu, mkarimu, mwenyekujua kufundisha, si mlevi, si mpiga watu, si mtu wa majadiliano, si mpenda fedha, mwenye kusimamia nyumba yake, si mchanga kiroho, mwenye ushuhuda mzuri nje, si mwenye kauli mbili, asiyetamani fedha ya aibu. Tito. 1:6 - 7.
Kumbuka:
Maadili yanatusaidia kuishi maisha ya mfano au kielelezo. Tazama
Tito. 1:8 - 9, 2Thes. 3:9, 1Tim. 4:12, 1Sam. 12: 2 - 5.
Unayoyafanya yatageuza watu zaidi ya yale unayoyasema.
Unavyoishi itasaidia kukazia mafundisho yako au pia kuyaondoa kabisa mioyoni mwa watu wanaokutazama.
Kumbuka:
Watu hujifunza zaidi kwa kuona, kisha kwa kusikia na kwa kiasi kidogo kwa yale mengineyo.
Maadili bora (mema) ni uamuzi na misimamo inayoweza kumfanya mtu binafsi au jamii iweze kuishi maisha ya haki, utaratibu na usafi.
Hebu tuangalie mfano wa watu (viongozi) hawa wawili:-
a) Sauli:
Yeye aliitwa na Mungu kuwa mfalme, alipakwa mafuta na kutumiwa na Mungu; Lakini:- 1Sam. 13:13 - 14
Alikuwa mtu wa kutenda bila kufikiri, aliweza kutoa sadaka kinyume na utaratibu wa Mungu.
Alikuwa mtu wa kutumia mabavu (ubabe - nguvu), kiburi kutotii na kupenda umaarufu. 1Sam. 15:12 - 26.
Na mwisho wa yote aliishia kuanguka na kukataliwa na Mungu. Tatizo lake alijiwekea maadili mabaya, ambayo hayakumpa Mungu utukufu.
1Sam. 15:10 - 11.
b) Nehemia:
Katika Neh. 5:14 - 19 hapa Nehemia anaonyesha msimamo wa haki, kama maadili (tabia) yake binafsi.
Alikusudia kufanya yaliyo mema na ya haki Mst.14
Alijitenga na watu walio wadhalimu (waovu) Mst.15
Alijitoa na kukaza macho yake kwenye kazi ya kuujenga ukuta - Mst.16
Nehemia alikuwa na uwezo wa kuwavuta wengine (nguvu ya ushawishi).
Alitoa mali zake kusaidia wengine - Mst.17
Alitanguliza maslahi ya wengine kwanza, badala ya faida yake - Mst.17 - 18.
Alionyesha kuwajibika kwa Mungu akimpa utukufu - Mst.19
Nehemia. 12:40 - 43.
Kukosa maadili mema kunajidhihirisha katika mambo yafuatayo:-
i) Maisha ya uasi kwa kiongozi kama vile wana wa Israel:
1Kor. 10:1 - 5.
Kutamani mabaya - 1Yoh. 2:15 - 17.
Kuabudu sanamu na shughuli nyingi - Mark. 4:19, Kut. 20:4 - 6.
Uasherati - Gal. 5:19.
Mawazo potovu.
Uhusiano mbaya (ugomvi) kati ya mke na mume (wanandoa).
Kukosa hekima katika kushauri/kushuriana.
Kumjaribu Bwana - Lk. 4:12
Manung’uniko - Hesabu. 14:26 - 27
Kiburi - Majivuno (kujiona wewe bora kuliko wengine) - Mith. 22:10.
Kumbuka:
Anatazamiwa kiongozi ya kuwa:-
“Alivyo kwa nje na ndivyo anavyotakiwa awe kwa ndani.”
“Vile anavyokuwa madhabahuni/mbele za watu anatakiwa awe pia mbele za familia yake.”
ii) Maisha mabaya katika fedha:
Kupenda fedha kuliko Mungu - 1Tim6:6 - 10.
Kutumia vibaya fedha za kanisa - Fil. 4:11 - 12.
Udanganyifu katika matumizi - Mith. 15:27, Rumi. 13:8.
Kutotoa fungu la kumi (Zaka) 10% ya mapato yako - Mal. 3:8 - 9, Ebr. 7:5 - 10, Zek. 5:1- 4.
Uzembe wa kutolipa madeni - Zab. 37:21, Mith.22:7
Kumbuka:
Hali hii inapozoeleka kwa kiongozi inasababisha hali ya kutokuaminika na kuonewa shaka.
iii) Matatizo katika ndoa:
Matatizo haya yanaweza kusababishwa na:-
a) Unafiki:
Nje kuonekana tofauti na hali halisi ya ndani.
Kuvaa sura isiyo yako.
Kuficha au kufanya siri shida na matatizo ya kindoa - Math. 23:27 - 28.
b) Kutokutatua matatizo madogo madogo ya ndani; na hivyo huzaa matatizo
makubwa - Lk. 16:10.
c) Kujilinganisha na watu wengine (ndoa nyingine):
2Kor. 10:12
Mwanandoa yeyote anayejilinganisha na mtu mwingine hana akili kabisa - zezeta.
Kumbuka: Tofauti zetu zinamfurahisha Mungu, siri ya ndoa bora ni msingi wake.
d) Dharau/Kiburi - 2Tim. 3:1 - 4.
e) Mawasiliano mabovu - Amos. 3:3
Kumbuka:
Adui hatakubali na hafurahi kuona mnaishi hivyo anachofanya ni kuwachafulia mawasiliano, msimpe nafasi. Efes. 4:27
f) Kipato/Fedha kidogo:
hili nalo huweza kuleta tatizo katika ndoa nyingi, hivyo kama mwanandoa jifunze kuridhika na uwezo wa mwenzi wako huku mkiweka mipango na malengo pamoja ili kuinua kiwango cha fedha na uchumi katika familia. Fil. 4:11 - 13.
g) Tabia za asili za mwenzi wako - Mith 30:11 - 14.
Hivyo ni vizuri wanandoa ukamjua mwenzako vizuri hasa juu ya tabia zake za asili - ndani, wakati wa uchumba huwezi kuziona tabia za ndani bali za nje.
h) Viwango vya tendo la ndoa
Mith. 5:15 - 19, Wimbo. 4:12 utoshelevu.
Swali la kujiuliza:
Je, unaujasiri wa kuhubiri mbele ya mkeo au mumeo na pia watoto wako? Kama unakosa ujasiri mbele yao basi, kunamambo yanayohitajika kupata ufumbuzi.
j) Kuacha kutunza familia kwa kisingizio cha kutingwa na huduma - Lazima
kuwe na uwiano, japo ni muhimu sana kumsikiliza na Roho Mtakatifu
kuliko kutii wanadamu -
1Tim. 5:8, Mdo. 5:29.
iv) Kuharibu huduma yako; kwa:-
Kupotosha neno la Mungu, kulighushi na bila ya kutumia kwa halali neno la kweli.
2Kor. 4:1 - 2; 2:17, 2Tim. 2:15.
Kuwatumia watu kwa kujinufaisha yeye binafsi badala ya kuwajenga na kuwaimarisha katika ufalme wa Mungu.
*Faida ya maisha na maadili mema ya Kiroho*
Ili uwe kiongozi, lazima uwe na wafuasi. Kuwa na wafuasi lazima wakuamini. Hivyo maadili bora ni ya lazima kwani yanakuwezesha wewe kiongozi katika mambo yafuatayo:-
Kurithisha (influence) tabia yako kwa wale unaowaongoza. Math. 26:73, 1Tim. 4:12.
Kutokuwa mtu wa kubadilika kama (kinyonga/popo).
Swali la kujiuliza;
Je, wewe ni yeye Yule kila wakati?
Je, jambo gani unafanya ambalo hutaki watu walijue?
Je, hii ndiyo tabia yako? 1Tim. 3:8.
Kumbuka:
Tabia yako isiyobadilika inagusa mioyo ya watu - Ebr. 13:7
Dhamiria kuwa mkweli na muwazi, usitafute kuonekana mzuri, bali uwe mzuri. Yer. 7:3 - 4.
Tabia huweza kujengwa na kubomolewa katika mambo madogo, hivyo dhamiria kuwa mwaminifu katika yaliyo madogo na utakuwa mwaminifu dhidi ya mambo yaliyo makubwa.
Unaweza ukabadili matendo yako ili yafuatane na kanuni za maadili mema au unaweza ukabadili kanuni za maadili zifuatane na matendo yako. Uchaguzi ni wako.
Dhamiria kuwa na nia ya kutumika kwa unyenyekevu, watu watakufuata wakijua nia na lengo lako ni kuwatumikia.
08. CHANGAMOTO ZA UONGOZI/KIONGOZI.
Hitaji kubwa la kanisa ni kupata viongozi bora wa kiroho watakaoweza kukabiliana na changamoto zilizopo nyakati hizi za mwisho katika kumwakilisha Kristo. Je, wewe ni miongoni mwao? - 1Tim. 3:1 - 7.
Swali: Utafanya nini wewe binafsi ili kuboresha uongozi wako?
Changamoto nyingine za kiongozi ni:-
Kiwango duni (cha chini) cha elimu na ufahamu sahihi wa neno la Mungu na mambo mengine - Mith. 3:13; 4:13.
Maisha yasiyo na ushuhuda mzuri. Math. 5:13 - 16
Kushindwa kufikia malengo/maono. Lk. 14:28 - 32.
09. MAFAO (FAIDA) NA THAWABU, GHARAMA NA ANASA ZA UONGOZI/KIONGOZI BORA WA KIROHO.
Uongozi una mafao/thawabu, gharama na anasa zake. Anasa ni pamoja na vikwazo vilivyomo.
I) {a} Mafao (Faida) & Thawabu ya Uongozi:-
1Thes. 5:12 - 13, Ebr. 13:17, 1Petr. 5:2 - 4, 1Kor. 9:10.
Heshima katika jamii - (Social Status).
Kutambuliwa na kueleweka - (Recognitation & Position).
Mapato (Material gain).
Mamlaka (Power & Authority).
Kuwa na mvuto kwa watu (Influence).
Mafao ya Kiroho (Spiritual Benefits).
Taji ya utukufu (Glorious Crown) Dan. 12:3 na 1Kor. 15:41.
Kupata kibali kwa Mungu na kwa wanadamu (God’s favour) - Mith. 3:3 - 4.
{b} Kuongoza vizuri mafao/faida ya uongozi:
Hesabu 27:12 - 23.
Ni jambo la msingi na lakuzingatiwa sana kwa kila kiongozi aliyepata kibali cha kuongoza kuyafanya haya:-
Uuone uongozi kama dhamana.
Uwe na nia ya Utumishi.
Jifunze kutofautisha kati ya mambo yako binafsi na cheo.
Kumbuka:
Panga maisha ambayo unaweza kuishi bila cheo.
Wekeza kwa ajili ya siku za mbele.
Uwe tayari kumpisha mwingine kuchukua cheo au nafasi yako.
Kumbuka:
Kuandaa Kiongozi/Viongozi (mrithi/warithi) watakaoendeleza mbio za uongozi hata wakati ambao hautakuwepo.
Mfano: Eliya, kabla ya kuondoka alimwandaa Elisha. 1Falme. 19:15 - 21.
Musa alimwandaa Joshua. Hesabu . 27:12 - 33.
Paulo alimwandaa Timotheo - 2Timotheo. 2:1 - 3.
Mwamini Mungu katika nafasi uliyonayo. Yosh. 1:6 - 9.
II) {a} Gharama za Uongozi.
Math. 5:11 - 12, Yoh. 10:11, Lk. 15:4, Yoh. 15:3, 1Sam. 17:35 - 37.
Kujitoa muhanga kwa ajili ya wengine (kondoo) - (Personal sacrifice).
Mateso ya kibinafsi - Kutokana na hisia mbalimbali.
Kukataliwa, kukatishwa tamaa, kuchekwa, kuzomewa, kulaumiwa, kudhalilishwa.
Matatizo ya ndoa na familia (kutengana kimajukumu)
kusingiziwa, upweke, shutuma, chuki, kusingiziwa, kusemwa, kuudhiwa.
Kuingiliwa katika maisha kwa mambo binafsi.
Kuwa tayari dhidi ya majaribu yatokanayo na fedha, zinaa (wanawake/wanaume) na utukufu (sifa) na matumizi mabaya ya madaraka n.k. 1Petr. 4:14; 2:20, Zab. 89:50 - 51.
{b} Kukabiliana na Gharama za uongozi.
Mjue sana Mungu na kumpenda - Fil. 3:8 - 10, Ayu. 22:21.
Jiandae kukabiliana na gharama hizo - Fil. 1:27 - 29.
Tumia muda wako vizuri kwa mambo yote, yaani uwe na kiasi.
Kol. 4:5, Efes. 5:15 - 16.
Uwe tayari kuwajibika.
Uwe mtu wa maombi, ili kumshirikisha Mungu mambo yote na kumtegemea.
Zab. 37:2 - 7, 23.
Jaa neno la Mungu - Kol. 3:16.
Jaa Roho Mtakatifu - Efes. 5:18.
Inua kiwango chako cha Ibada - Yoh. 4:23 - 24.
Kuishi maisha safi - Matakatifu yenye ushuhuda mzuri. Math. 5:13 - 16.
III) {a} Anasa au majaribu (vikwazo) vya uongozi:
Anasa ni mambo ya starehe yasiyo ya lazima.
Uongozi huambatana na anasa zake ambazo ni mitego na majaribu kwa kiongozi.
Baadhi ya majaribu hayo ni:-
Kujiona umefika juu ya kilele (kiburi) - Isa. 14:13 - 14, Mith. 29:23.
Kushindwa kuwa na maono - Mith. 29:18.
Kuacha kuwa mfano wa kuigwa.
Kutumia madaraka/Uongozi kwa faida binafsi.
Kukataa kujipima mwenyewe - Gal. 6:4 - 5.
Kuridhika na utendaji usioridhisha.
Kutumia vibaya madaraka/uongozi kwa watu unaowaongoza.
Zinaa/Uzinzi/Uasherati.
Kujisifu na kujiinua (sifa) - Fil. 2:3, 14:16.
Wivu.
Kutokujali familia.
Kukosa motisha na kuahirisha mambo.
Kujisikia huwezi na hufai (kujidharau na kujikataa) - Hesabu. 13:32 - 33.
Kupoteza dira ya uzima wa milele.
Fedha - 1Tim. 6:10. na yanayofanana na hayo.
{b} Namna ya kukabiliana na Anasa, mitego na majaribu ya Uongozi:
Soma maandiko haya:- 2Tim. 4:15 - 16, 1Thes. 4:1; 5:17 - 18, Fil. $:6 - 7. Hivyo ni lazima:-
Kukaa katika maadili mema ya Kikristo.
Kudumu na kutii neno la Mungu.
Kudumu katika maombi - Mith. 16:3, Lk. 18:1 -
Kuhusisha mambo yako kwa walio karibu nawe, watu au timu yako ya Uongozi kwa ushauri. Mith. 20:18, Mith. 15:22.
10. SIRI YA MAFANIKIO YA UONGOZI/KIONGOZI WA KIROHO:
Pamoja na kuwa na maadili bora mambo yafuatyo ni muhimu sana kwa kiongozi ili aweze kufanikiwa:-
i) Kumwamini na kumpenda Mungu - Yoh. 14:1, 12, 21, 23.
ii) Kufanya mapenzi ya Mungu - Math. 7:21, Efes. 5:10, Yoh. 5:24.
iii) Maombi - Lk. 18:1, 1Tim. 2:1, Lk. 6:12, Mark. 1:35 - 39, Ebr5:7 - 10, Ezr. 8:21 - 23.
iv) Kuwa na mipango mizuri - Lk. 14:28 - 32, 1Tim. 3:15.
v) Kujali rasilimali ulizonazo pamoja na muda na watu - Kut. 10:24 - 26, 8, 9, Lk. 22:35 - 36, Efe. 5:15 - 16.
vi) Mahusiano bora na wengine wanaokuzunguka - Ebr. 12:14 - 15, Yoh. 13:34 - 35..
vii) Usiridhike na ulichonacho tamani kujifunza toka kwa wengine - Mith. 2:3 - 6, Mith. 12:9 -
11. KIONGOZI MWENYE MAONO NA MALENGO:
Mithali 29:18.
Ipo tofauti kubwa kati ya Maono na Malengo
(A) MAONO NA MALENGO:
MAONO:
Ni ule uwezo wa kupata picha ndoto/dira/ufunuo ya mambo ya siku za mbele; ambapo MALENGO: Ni ile namna ya kuyatekeleza hayo maono uliyoyaona au uliyoyapata.
Ni kufanya safari toka kwa unayoyaona sasa kwa yasiyofahamika na kuyaona kama yapo katika uhalisia.
Watu wengi wanakwama kwani wanadhani kitu cha muhimu ni fedha, hapana cha kwanza ni kuwa na maono pesa ije iingie kwenye hayo maono. Pesa bila maono itapukutika yote. Rejea kwa Yusufu aliingia Misri kama mtumwa, hana kitu, lakini alikuja kuwa mtawala kwa sababu alikuwa na maono.
Mfano:
Nuhu aliona mapema gharika juu ya uso wa nchi akawaonya watu wake. Mwa. 6:13 - 22.
Yusufu aliona miaka saba ya njaa kabla ya kutokea. Mwa. 41:28 - 30.
Musa aliona nchi ya ahadi - Kut. 3:3 - 9.
Nehemia aliona Yerusalemu mpya - Neh. 1:2 - 6, Neh. 2:3 - 5..
Paulo aliona Makedonia inahitaji injili Mdo. 16: 9 - 10.
Swali:
Je, wewe unaona maono gani juu ya:-
{a} Kanisa? (b).Familia yako? n.k.
Kumbuka:
Mtu mwenye maono siku zote hufuatwa na kutafutwa na watu, bali mtu asiye na maono siku zote huwa mtu wa kufuata na kutafuta watu. Soma Mwanzo. 45: 3 - 10; 50:20 - 21.
(B) BAADA YA KUONA MAONO:
Ni lazima mambo yafuatayo yafanyike ili maono yawe mambo au kitu halisi na wala sio ndoto za kupita tu.
Kuhamasisha watu; Ili kuyatimiza mambo uliyoyaona. Mfano, Musa alihitaji kuwaona wazee wa Israel kwanza - Mwa. 3:16 - 18, 4:29 - 31. Hivyohivyo na Nehemia pia - Neh. 2:17 - 18.
Kuweka malengo: Yaani mipango ya utekelezaji ili kuyafanikisha maono lengwa/ husika.
Kumbuka:
Pasipo maono watu hujiendea - hupuyanga hovyohovyo na mwisho hupotea na kuangamia; Na pasipo malengo na mipango mizuri watu watashindwa kuyafikia maono, na hawawezi kuhamasika tena kuendelea mbele kuyatekeleza.
Hatimaye kila mtu atafanya anavyoona inafaa machoni pake mwenyewe. Amuzi. 21:25.
(C) MSINGI WA BIBLIA KUHUSU KUWEKA MALENGO:
Yesu alitoa mfano wa mjenzi wa mnara na mfalme aendaye vitani. Lk. 14:28 - 32.
Paulo alitoa mfano wa mwanariadha, mpiganaji ngumi, mkulima, mwanamichezo na Askari - 2Tim. 2:3 - 10, 1Kor. 9:24 - 26, Fil. 4:14, 2Tim. 4:7.
Mjenzi katika kuweka malengo inamlazimu kuchora ramani, kukusanya vifaa na rasilimali zingine, kisha kuanza kujenga hatua kwa hatua.
Mpiganaji kabla ya vita (pambano) hujiandaa, huandaa majeshi, vifaa, silaha na njia (mbinu) za kuendelea na hivyo hujipanga kikamilifu kabla ya yote, kwa nia ya kupigana.
Kumbuka:
Mpango wa Mungu wa wokovu ulikuwa na malengo na mipango yake ya utekelezaji.
Hivyo Mungu aliandaa mtu mmoja ambaye ni Ibrahimu, Baba wa Imani.
Kisha Taifa la Israel kuwepo.
Manabii/Yesu kuzaliwa awe mkombozi wa ulimwengu.
Mitume/Roho Mtakatifu/Kanisa/ Hatimaye wokovu wa milele (Uzima wa MIlele).
(D) FAIDA YA KUWEKA MALENGO NA MIPANGO:
i) Huwezesha kuwa na mwelekeo mzuri wa mambo au kazi katika maisha.
Kumbuka:
Watu wote wasio na malengo hawafiki popote.
Malengo na mipango hufanya maisha yawe ya maana na huweka mwongozo wa maisha. “Kama hujui unakokwenda, njia yoyote itakufikisha huko usikokujua.”
Hivyo kukosa malengo na mipango huo ni upofu, na shimoni lazima utatumbukia tu - Math. 15:14
Kumbuka:
“Ukilenga hewa utafanikiwa kupiga shabaha hiyo, na hakuna anayelenga hewa akaikosa.”
ii) Huhamasisha mambo kufanyika:
Viongozi wengi waliofaulu vizuri wanakiri kuwa walihamasika na malengo waliyokuwa nayo, na kujiona wakitembea kuelekea katika malengo hayo.
Ni malengo yanayowaelekeza ni wapi wawekeze na kutoa vipaumbele katika mali na rasilimali walizonazo na pia nguvu zao.
iii) Humfanya mtu kuwa na Tabia (shauku) ya kutaka kuona matokeo.
Malengo na mipango humfanya kiongozi awe na hamu/ shauku ya kuona matokeo ya kazi anayoifanya na maendeleo yake yalivyo.
Malengo yanamfanya mtu kuweka mkazo katika matokeo, badala ya shughuli zinazofanyika.
Malengo na mipango humsaidia kiongozi
Kupima utendaji na shughuli (huduma) yake.
Kujua umekwenda umbali gani? (napiga hatua au hapana)
Kuwajibika.
Kutathimini kazi mara kwa mara na kuboresha utendaji wake.
Gal 6:4 -5
Kumbuka:
Viongozi waliofaulu ni watu ambao wana malengo kwa siku za mbele. Si watu wa kushughulikia matukio tu au watu na mambo yaliyopita.
Huwa hawasubiri mambo yaotokee na ndipo wafanye kitu, bali ni watu wanaojitahidi kutimiza mambo, kwa sababu:-
i) Wana maono yaliyo wazi.
ii) Hujiwekea mipango na ratiba ya kutimiza maono hayo.
iii) Wanawajibika katika kufuatilia malengo waliyojiwekea.
vi) Huvumilia wakati maono, malengo na mipango inapokutana na vikwazo
mbalimbali na kutotimiza malengo aliyokusudia.
v) Hupata ufumbuzi na kubuni njia ya kuendelea mbele si kurudi nyuma na kukata
tamaa.
12. AINA YA VIONGOZI/UONGOZI.
Kuna viongozi wa aina nyingi, leo tuangalie mbili ambao ni:
Wale wanasababisha mambo kutokea na
Wale wanaosubiri mambo yatokee.
I} sifa za viongozi wanaosababisha mambo yatokee.
Wana mtazamo wa mbele (wana ndoto, maono, malengo, mipango) Mith. 29:18, Mwanzo 37:5-11.
Wako tayari kupanga mipango, na kuona jinsi gani watakavyoyatimiza malengo/maono hayo. Mwanzo 41:1 – 44
(Mst. 25 – 40)
Wanaweka mikakati ya kuzuia matatizo yatakayoweza kutokea. Mwz 41:33 – 36.
Hawakati tamaa na pia ni hodari na jasiri. Hesabu 14;6 – 9’13:30
II} sifa za viongozi wanaosubiri mambo yatokee.
Hawafanyi chochote/hawajishughulishi mpaka mambo yatokee.
Hutumia muda mwingi kushughulikia matukio. Hesabu 13:31 -33
Ni wazima moto na hutumia muda mwingi kuzima moto bila kujiuliza chanzo cha huo moto kutokea. Math 9:32 – 33.
Kumbuka:
Tofauti kubwa kati ya viongozi wa aina mbili hii ni Uwezo katika malengo na kujishughulisha na mipango pia mikakati mbalimbali katika kutimiza maono yaliyopo.
Kumbuka:
Maono, malengo na mipango lazima iwe Smart (safi), yaani iwe na sifa hizi:-
Spirit led & specific - Uongozi wa Roho Mtakatifu na yenye shabaha (yaliyo wazi – bayana).
Measurable – kupimika/yenye kutathiminika.
Attainable – yenye kufikika.
Realistic – yawe halisi
Time targeted – muda maalum
Soma Lk. 4.:18 – 22, 1Tm. 4:7, 1Kor. 9:24 – 26
Maono/mipango/malengo yanaweza kushindikana kufikiwa kutokana na sababu zifuatazo:-
Hayakuwa na shabaha (bayana) maalumu.
Hayapimiki.
Hayafikiki kirahisi.
Hayako halisi kibinadamu.
Hayakutengewa muda maalumu, yangekuwa na muda yangeweza kuhimizwa na kukamilishwa haraka na hivyo kufurahia matokeo yake.
Kumbuka:
Maono yako yafafanuliwe kwa maneno yako, maneno yako yazae matendo na tabia, malengo, mipango na mikakati.
Hatimaye yataonekana matokeo kamili (halisi) kutokana na mawazo uliyonayo> bila hivyo mawazo/maono uliyonayo yatabaki kuwa ndoto tena za mchana.
Hivyo kiongozi wa kiroho lazima kuwa na mtazamo wa ki Mungu, kama vile Mungu mwenye Enzi alivyo na maono thabiti tangu mwanzo hadi mwisho wa kazi yake katika ulimwengu huu na ule ujao.
Mipango na mikakati yake ya wokovu imekuwa na ushirikishwaji wa mwanadamu na kwa uwazi kabisa. Rumi 8:28.
Uongozi wa kiroho unabeba sura ya Mungu mwenyewe kwa wana wa Mungu wanaotegemea. Mith. 16:4, Rumi 8:14, Yhn. 15:6, Isa. 14:24, Math. 28:20
13. KIONGOZI ANAYEFAA KUIGWA NA WATU WENGINE.
Zifuatazo ni baadhi ya sifa/vigezo apasavyo kiongozi kuwa navyo ili watu wengine waweze kuiga kutoka kwake.
Watu huvutiwa na kumfuata kiongozi aliye na:-
I} Maono.
Kiongozi asiye na maono hafai kuwa kiongozi. Mungu humtumia mtu mwenye maono na mipango safi. Mfano Musa, Joshua n.k.
Hivyo kiongozi lazima ujue unakwenda wapi na Mungu anataka nifanye nini? Mith. 29:18
II} Mfano/Kielelezo: 1Tim 4:11 – 12, 2Kor. 3:2 -3
Mtume Paulo hakusita kuwaeleza watu kuwa wamfuate/wamuige yeye anavyofanya. 1Kor. 11:1, Fil. 3:17, Fil. 4:9, 2Thes. 3:7, Lk. 14:25.
Kumbuka:
Kuacha/kushindwa kuongoza kwa mfano mwema ndio kuzaliwa hadithi za kale, utasikia mtu anasema, enzi zetu, wakati, miaka ile tulifanya hiki na kile, lakini leo hawezi, hilo tayari ni tatizo, umeshindwa kuwa kielelezo kizuri.
III} Uadilifu: 1Sam 16:7 –
Uadilifu ni suala linalohusika na moyo wa mtu mwenyewe (tabia) yake.
1Sam. 16:7, Zab. 78:72
Kumbuka:
Unapopoteza uadilifu umepoteza uthamani na ubora (kibali) cha uongozi wako.
Uadilifu unajengwa kupitia; kufanya (kutenda) na kutekeleza ahadi na kujitoa kikamilifu.
IV} Neno la Mungu: Ebr. 4:12, 2Tim 13:17, Mdo 6;2, Ebr 13:7, Kol. 3:16, Yh 1:1 – 14.
Viongozi ni wasomi wa neno (Leaders are Readers) kwa sababu, Mtumishi wa Mungu hutegemea neno la Mungu, kumuongoza Zab. 119:105 na kumpa nguvu (chakula)
Math 4:4, Ay 23:12.
Je unafanya nini ili kujilisha neno?
Unafanya nini katika kuhakikisha wengine wanakula (pata) neno la Mungu?
V} Maombi: mdo. 6:4, Lk. 5:16.
Kama kiongozi lazima ujitoe kikamilifu katika maombi na kulihudumia neno.
Mara zote mwanadamu hutafuta njia zilizo bora zaidi.
Mungu naye anatafuta mtu (kiongozi) bora aliyeshujaa na hodari katika maombi.
Mfano Joshua akiwa vitani Kut. 17.
VI} kiongozi aliyejaa roho mtakatifu:
Mdo 6:3, Yhn. 15:5, 2kor. 3:5 – 6, 2kor 13:14, Kol.1:1 – 29.
Sisi (viongozi) bila roho mtakatifu hutuwezi kufanya chochote.
Kumbuka:
Popote palipo na kiongozi aliyejaa Roho Mtakatifu elewa kuwa nyuma yake yupo Mungu 2kor 3:5 – 6.
VII} Mwenye Bidii na Kazi: 1Thes. 5:12 – 13, kut. 2:15
Kiongozi bora, Mtumishi lazima awe na bidii ya kazi za mikono na huduma ili watu wamkubali. Rumi. 12:8
VIII} Mwenye Imani: Ebr 13:7, 11:1,6, Ebr. 10:38, Rumi 1:17.
Mwanafalsafa mmoja alisema “Ni bora kuwa na simba mmoja anayewaongoza kondoo elfu moja, kuliko kondoo mmoja kuongoza simba elfu moja.”
Kiongozi bora lazima awajibike kuwaongoza watu katika kumwamini Mungu na kumtegemea yeye (Mungu).
IX} Anayekua/Ongezeka (Mwenye Kujifunza) Yh. 8:31 – 36.
Kiongozi hayuko kamili ila mara zote yupo kwenye mchakato wa kujifunza mambo mapya katika maisha yake ya Imani.
Kumbuka:
Kiongozi aachapo kujifunza na kukua ndipo mwisho wake wa kuongoza hufika.
X} Maisha Safi ya Nyumbani: 1tim. 4:12 -16.
Mtu mmoja alisema, “ikiwa haifai nyumbani, usiiuze nje.”
Ukishindwa kusimamia nyumba yako, yaani mke/mume na watoto tayari umeshindwa kuwa kiongozi bora wa kiroho ( ki – kristo).
14. Misingi ya Kiongozi/Uongozi wa Kiroho.
Misingi ni nguzo ambazo kwazo kiongozi wamejengwa au anajengwa ili kufaa katika uongozi:
a} Kujitoa kwa
Kristo (Bwana – Mungu) – 2Kor 8:5
Watu – 9yhn 3:16
b} Utii: mwz. 12:1 – 4
Neno utii limeunganishwa na Bwana wa majeshi. Hii lugha ya kijeshi wajibu wa askari ni kutii kutekeleza amri kwanza na maelezo baadae Efo. 6:1- 2.
c} Uaminifu: 1kor. 4:1 – 2.
Kipimo cha Kiongozi ni Uaminifu Katika
Maagano.
Mahudhurio.
Muda.
Matokeo.
Ibada n.k.
d} Tabia za Kiroho/Nidhamu za Kiroho: Mdo 6:4
Maombi
Kusoma na kutafakari neno.
Ibada
Matokeo
Utumishi (Huduma)
Kumbuka:
Nguvu zetu katika huduma inategemea muda ninaokaa mbele za Mungu, kuomba na kutafakari neno lake.
e} Uwajibikaji: Mark 6:7, 30
unapokuwa kiongozi kuna maneno ya:-
Kuagiza.
Kutumwa (kuagizwa jambo)
Amri (hakuna kuhoji ni kutekeleza tu).
Kumbuka:
Ni lazima kutoa taarifa kwa mkuu wako ( Mchungaji)
Lazima uwe mtu wa mawasiliano.
f} Kuambatana: 1Sam. 18:1, 1Kor. 1:10, Math. 12:30, Ruth. 1.14 – 18.
Kuambatana ni kushikana na viongozi wenzako ili kutompa nafasi ibilisi (Adui) shetani kutushinda. Efe. 4:27.
Kutokuwa kigeugeu Mith 26:21.
Misingi ya kuambatana: 1kor. 1:10
Kunena mamoja.
Kutokuwa na faraka – matengano
Kuwa na nia moja.
Kuwa na shauri moja.
Siri ya kufikia hatima yako njema salama katika uongozi ni lazima ujifunze kuambata na wenzako vizuri, bila hivyo hutafika mbali (itakuwa kama mbio za panya sakafuni).
Nikinukuu maneno ya makamu Askofu Mkuu wa TAG Dr Magnus Mhiche alisema siku moja kuwa “ukitaka kwenda mbali nenda mwenyewe (peke yako), lakini ukitaka kwenda mbali zaidi jifunze kwenda (kuambatana) na wengine. Mfano: Gehazi alishindwa kufikia hatima yake akiwa na nabii Elisha baada ya kujitenga kushindwa kuambatana naye. 2Falme 5:20 – 27.
Pia Akani aliuwawa kwa kupigwa mawe maana hakuweza kuambatana na Joshua. Yosh. 7:9 – 25.
Kumbuka:
Ili ufike (mwisho) hatima yako lazima ujifunze kuambatana na wenzako maana wao ni walinzi wako.
Dawa/tiba ya mtu asiyependa kuambatana na wenzake ni kumtupa nje kumwondoa. Mith 22:10, Yosh. 7:1 – 25 kwani bila kufanya hivyo wote mtapigwa na adui wala hamtaweza kusimama tena.
g} Kupokea Maonyo: Mhubiri 4:13
Kiongozi bora wa kiroho lazima ajifunze kupokea maonyo/awe tayari kuonywa na kusahihishwa pale atakapo kengeuka/kosea.
H} Kuwa Balozi Wako (Mchungaji)
Jifunze kumtaja vizuri au kumnena vema kiongozi/mchungaji wako (Mkuu wa kituo) mbele ya watu pia jaribu kunukuu na kurejea mafundisho yake ukionyesha jinsi yalivyokusaidia na waimarishe watu kutokana na mafundisho yake na maono ya Kanisa hasa pale upatapo nafasi kusimama madhabahuni au katika idara yoyote na kipindi chochote Kanisani na siyo kumpinga (kumponda) na kuanzisha kitu kipya.
15. Lugha ya Kiongozi/Uongozi.
Lugha ni njia ya mawasiliano. Na ili adui awaweze na kuwashinda ni lazima kwanza aharibu miundo mbinu yenu ya mawasiliano.
Lugha pekee ya kiongozi ni KUAMBATANA. Tazama Ruth. 1:14 – 18, Amos. 3:3 na 1Sam 18:1.
16. Sifa za Jumla za Kiongozi/Uongozi wa Kiroho.
Kiongozi wa kiroho lazima awe na:-
Uwezo wa kuongoza
Mcha mungu
Mkweli
Achukie mapato ya udhalimu (utapeli) yasiyo halali (rushwa).
Mtu mwema/mwadilifu.
Amaanishe anachosema na aseme anacho maanisha.
Ajae roho mtakatifu.
Awe mvumilivu
Awe na maono (Mith. 29:78)
Apende ibada
Awe mtunza siri.
Awe mbunifu Mw 30:25 – 43, 2:15
Awe na hekima.
Awe mtu wa kujitoa
Asiwe mtu wa udhuru
Awe mnyenyekevu 1Pt 5:6, Math 8:21 – 22, 1Flm 19:20.
Awe mcheshi
Aishi maisha ya uanafunzi. Yhn. 8:31 – 36.
Anayekubali changamoto na kufanya uamuzi.
Awe amezaliwa mara ya pili. Yh. 3:3 – 8.
Awe na huruma. Lk. 7:12 – 13, Math. 9: 35 – 38.
Awe mtu mzima katika imani, siyo mchanga. 1Tim.3:6
Anayekubali ushauri. Kut. 18:13 – 27.
Awe na ufahamu sahihi wa neno la Mungu na mambo mengine Mith. 2:3 – 6. Soma Pia: Kut. 18:21 – 24, Mdo 6:3, Rumi 12:6, Mith 11:30, 2Nyakati 1:11 – 12, 1Tim 3:1 – 13, 1Falme 3:5 – 28.
17. Wajibu wa Jumla wa Kiongozi wa Kiroho.
Mdo 20:1 – 38, Yhn 10:11 – 15.
Wajibu ni majukumu (kazi) apaswayo kiongozi kuyafanya kwa nguvu zake zote ili kuyatimiza malengo yake.
Baadhi ya majukumu/wajibu wake ni :-
i} Kujitunza nafsi yake: 1Thes 5:23
Nafsi imebeba:-
a} Akili
b} Makusudi (nia)
c} Hisia
Mith. 4:23, 1Kor 15:33 – 34
Hivyo kama kiongozi lazima uitawale nafsi yako mbele ya hao unaowaongoza.
ii} Kulitunza Kundi
Ni wajibu wa kiongozi kulilinda, kulichunga na kulihakikishia usalama kundi ninaloliongoza dhidi ya:-
a} Mbwamwitu wakali: Watumishi waharibifu ambao kondoo siyo wito wao.
b} Imani potofu: Mafundisho ya uongo (Mashetani).
Kumbuka:
Hili litawezekana pale tu kiongozi atajitoa kwa kufundisha watu wake Elimu sahihi ya Imani (Neno la Mungu) – (Sound Doctrine).
Tunayapinga mafundisho ya uongo kwa kufundisha kweli ya Mungu. Yuda 1:3 – 6, Yhu 8:31 – 36, Hosea 4:6, Mith. 11:9 na Mith. 21:16
Kumbuka:
Kanisa linaangamizwa kwa kukosa maarifa, Elimu sahihi ya neno la Mungu. Hosea 4:6, Mith. 21:16.
Hali kadhalika Kanisa linapona kwa maarifa. Mith 11:9, Yhn 8:31 – 36.
Kumbuka:
Kanisa linajengwa/imarishwa na kuponywa kwa mafundisho, mafafanuzi ya neno la Mungu. Za 119:130 na wala siyo Mahubiri, kukemea maombezi.
Kumbuka:
Shetani haogopi mahubiri wala maombezi au makemeo bali anaogopa ufahamu unaomjua Mungu. Ay.22:21, Lk. 4:1 – 14.
Hitimisho:
Mungu haangalii uliipataje nafasi hiyo ya uongozi, yeye anaangalia kusudi lake la hiyo nafasi linatimia kikamilifu.
Elewa kuwa Roho Mtakatifu ndiye aliyehusika kuwatumia hao waliokuchagua au aliyekuteua katika nafasi hiyo ya uongozi uliopo.
Hivyo sasa, kuwa huwajibiki kwa mtu (mwanadamu) bali kwa Mungu moja kwa moja. Mdo. 20:28.
Elewa, kuwa kutokutimiza wajibu wako kama kiongozi haumkomoi mtu bali unatafuta ugomvi na Mungu aliyekuwa kuwa mwangalizi, kiongozi na msimamizi wa kundi lake.
Zingatia:
Itakuwa heri kwako, Bwana akikukuta ukidumu katika kuwahudumia watumwa, watu wake kwa Uadilifu na Uaminifu wote na kwa unyenyekevu kabisa; atakuweka kuwa juu ya vitu vyake vyote na usipofanya hivyo atakukatakata vipande vipande na kukutupilia mbali. Math. 24:45 – 51.
Uishi Milele.
2Kor 13:14
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Ahsante sana mchungaji, nimefurahishwa sana na somo hili na nitaelendelea kujifunza
ReplyDeleteRashid Songoro
Mkurugenzi CA
TAG msufini - kigoma
http://revenuebrust.com/?refcode=19732
ReplyDeleteSalam sana mtumishi wa Mungu, Bwana Yesu atukuzw. Nimesoma na kuelewa somo la uongozi hapo juu. Kuna haja kwa watumishi kuboresha uongozi wao kiroho kukabiliana na changamoto za siku za leo kwa kufunga na kuomba Mungu atoe mwongozo wa kiroho kwa kanisa. pili kuandaa viongozi watakao endeleza kazi hii baadaye. Barikiwa sana Mtumishi.
ReplyDeleteNi mimi Mch Noel Mollel - UPCT MOSHI
Thanks so much for all of your attention to this matter and I will be in the area around the house with all saints and then we will be there be blessed God servernt
ReplyDeleteHi. Mtu wa MUNGU hongera kwa masomo mazuri na juhudi yako kubwa nimeipenda sana kazi yako naomba kama utaniruhusu nifundishe masomo haya na kama ndivyo unipe kibali na uwezo wa kunakili na kuprint copy. ndimi mjoli wa BWANA Joshua Mosha . mtumwawayesu@gmail.com Kisiwani Mafia. MUNGU AKUBARIKI SANA KARIBU KISIWANI MTU WA MUNGU
ReplyDeletePastor Mungu wa mbinguni akubariki Sana kwa fundisho hili juu ya uongozi was kiroho.Neema za Mungu ziwe juu yako.
ReplyDeleteAsante sana mtumishi nimebarikiwa sana naomba kupata pdf zake
ReplyDeleteI am so happy with your lesson I vividly learnt and enjoyed your the matter of administration Amen.
ReplyDelete