IJUE IBADA YA KWELI.
Yohana 4:20-24
MWANDISHI:
PASTOR. SONGWA .M. KAZI
GLORY TO GLORY CHRISTIAN CENTRE
TAG –GGCC FOREST KONGOWE,
S.L.P. 70983, DSM
SMU: 0757-567-899 /
0789-567-899
Whasap: 0719-968-160
Blog: www.lcm2014. blogspot.com
YALIYOMO:
1.
Maana ya ibada.
2.
Aina za ibada.
3.
Jinsi
ya kumwabudu Mungu katika roho na kweli.
[ method of worship ].
4.
Sura , picha au mwonekano wa ibada inayo kubalika.
5.
Sifa za jumla za mwabudu .
6. Ibada isiyo kubalika mbele za Mungu.
7. Tofauti kati ya Huduma na Ibada
SHUKURANI
· Kipekee kabisa na mshukuru sana Mungu wangu BWANA Yesu Kristo
aliye niita kwa wito mtakatifu kwa kuniokoa na kunitenga kwa ajili ya utumishi
katika ufalme wake.
· Pili; namshukuru Yesu wangu kwa kunipa mke mwenye busara Miriam
Songwa Kazi na wanangu Meshach, Prince na Amani kwa maombi na uvumulivu wao
kwangu pindi walipo nikosa nikiwa katika maandalizi ya kazi hii njema unayo
isoma sasa.
· Tatu; ninazo shukurani zangu nyingi kwa baba na rafiki;
Mchungaji wangu kiongozi Askofu Victor A.
Tawete na familia yake kwa ushauri , kunitia moyo, kuniombea na kwa
mafundisho yake yaliyo kuwa na mchango mkubwa kwenye maandalizi ya kitabu hiki.
· Nne; nina washukuru kipee wazazi wangu, rafiki zangu kipenzi na
watenda kazi pamoja nami katika kazi ya Injili ya ufalme wa Mungu; wana Life
Changing Ministry International [ LCM ] na wachungaji wote rafiki zangu kwa
maombi yao na ushauri wao. Mungu awabariki sana.
WASIFU WA MWANDISHI NA
KITABU:
o Mchungaji Songwa M. Kazi , ni mtumishi wa Mungu ambaye amekuwa
akifanya huduma za Mikutano ya Injili, Semina, Ushauri na Maombezi kwa watu wengi ndani na nje ya nchi ya
Tanzania kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Ni mtenda kazi makini wa Injili ya Kristo
mwenye maono ya kuleta matengenezo, uamsho na urejesho katika mwili wa Kristo
ulimwenguni bila kuwa na mipaka ya udhehebu.
Kwa sasa ni Mchungaji Msaidizi katika kanisa la GLORY TO
GLORY CHRISTIAN CENTRE
[ TAG- GGCC FOREST KONGOWE, DSM
]; Pia
ni mkurugenzi wa Huduma iitwayo
Life Changing Ministry International [ LCM ] yenye makao yake makuu Dar -es -Salaam
.
o Kuhusu Elimu, anayo elimu
ya Biblia kutoka AFRICAN LEADERSHIP
INTERNATIONAL [ AL ] ngazi ya cheti na kwa sasa anachukua masomo ya Shahada ya
Kwanza katika Huduma, Utawala na Uongozi katika chuo cha T-NET INTERNATIONAL.
o Mbali na Huduma hizo, ni mwandishi wa vitabu vya kiroho vyenye
mafundisho shadidi katika ulimwengu wa sasa. Katika kitabu chake cha “ IJUE
IBADA YA KWELI” , Mchungaji. S. Kazi , kwa kweli ameweka mwongozo muhimu wa namna
mwamini anavyoweza kuuridhisha moyo wa Mungu kwa ibada ya kweli tena ya rohoni.
Hivyo ukiwa na IJUE IBADA YA KWELI, utakuwa umejiweka kwenye nafasi sahihi ya
kutoa manukato safi na mazuri mbele za BWANA wakati wa ibada, yaani kutoka
chini ; kwetu sisi kwenda juu kwa BABA ambako hutoka rehema, neema na
Baraka.
o Mchungaji Songwa Kazi ana mke na watoto watatu wa kiume.
§ Na; Ev. Abraham JC. Magoma, Mwanatheolojia wa karne ya 21 , mwalimu
wa chuo cha Biblia na Katibu Mkuu wa huduma ya Life Changing Ministry
International [ LCM ].
UTANGULIZI:
Je,
umewahi kujiuliza kwa nini unakwenda kanisani?
Najua wengi watajibu kuwa , wanakuja au
wanakwenda kanisani kuabudu; kitu ambacho ni kweli kabisa. Ila cha ajabu
leo, asilimia kubwa ya waamini hao
hawaji kanisani kwa lengo hilo, bali wengi wao wanakuja kanisani kwa lengo la
kupokea tu; yaani hawapo kiibada bali wapo kihuduma zaidi. [ they are not after
worship but they are ministerial minded / they are after receiving .] Pia wengine
hudhani kuwa kuabudu ni kuimba nyimbo fulani
za polepole kwa sauti ya upole na kusifu ni kule kuimba nyimbo fulani za
harakaharaka. Kitu ambacho siyo kweli hata kidogo!
Kumbuka kuwa, nyimbo, muziki na mahubiri siyo
ibada ; bali ni funguo tu za kutupeleka kwenye ibada. Ibada si jambo la mara
moja au kipindi fulani maalumu; bali ibada ndiyo aina au mtindo wa maisha ya
kila siku ya mwamini. Jumla ya maisha
yako ndiyo ibada yako; yaani kile kinacho chukua nafasi kubwa katika muda wako,
pesa zako, mazungumzo yako , moyo wako, akili zako na nguvu zako
SURA YA KWANZA:
MAANA YA IBADA.
o
Ibada ni heshima [ respect ] inayotolewa na mtu kwa
bwana wake kwa lengo la kumfanya ajisikie tu vizuri. Elewa wazi kuwa neno ibada halimanishi kuwa ni takatifu bali kile
unachokiabudu ndicho kitakacho amua na kutueleza aina yako ya ibada.
Ibada ni kitendo cha kuanguka chini ya miguu
ya bwana wako na kuibusu miguu yake au
mikono; tendo amabalo Wagiriki [
wayunani ] huliita ; proskuneo .
Katika mazingira haya; tunaweza kusema
kwamba:
Ibada ni utii
[obedience] – yaani kufanya au kutekeleza jambo ulilo agizwa bila kuhoji.
Ibada ni sadaka inayotolewa kwa Mungu.
Heri kutoa kuliko kupokea; Matendo 20:35b
Ibada ikiwa kama sadaka hulenga maeneo makuu
matatu ya kutoa; ambayo ni:-
i. Kujitoa
mwenyewe [ giving your self ]:
“Basi,
ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu
iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Warumi
12:1
ii. Kutoa
Mambo Ya Ujazayo Moyo [ Heart Attitudes
]:
“Na
huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake , akamwomba BWANA akalia sana.
Hana
akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni,
mimi sikunywa divai wala kileo ila nimeimimina roho yangu mbele za BWANA.” 1Samweli 1:10, 15
iii. Kutoa
Mali Zako [ Giving Your Possessions ] :
“ Bali
utamkumbuka BWANA, Mungu wako,
maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara
agano lake alilowapa baba zako, kama
hivi leo.” Kumbukumbu la Torati 8:18. Pia katika
Zaburi 24:1 maandiko husema,
“Nchi
na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani
yake .” Mtume Paulo naye alisema hivi ; Au
hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho
Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu
wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili
yenu. 1Wakorintho 6:19-20
Kwa
maana hiyo, msingi bora wa utoaji wa
ibada kama sadaka ni NIA yako ya utoaji. Mungu haangalii jinsi unavyo
jitoa sana au kiasi kile unachokitoa
mbele zake , bali ana angalia hasa nini NIA
YAKO juu ya kutoa na kujitoa kwako na pia anangalia
ulichobakisha baada ya kutoa.
ü Luka 21:1- 4, Marko 12:41-44 [ utoaji wa
sadaka ]
ü Wafilipi 2:4-5 [ nia
ya Kristo ]
Tuwe na nia ya Kristo ambayo ni utumishi . Marko
10:45 .
· Tambua kuwa wewe mwenyewe na vyote ulivyo
navyo siyo mali yako; wote na vyote uvionavyo ni mali ya Roho Mtakatifu [ Mungu
], hatuna chakujivunia kuwa ni chetu. Ayubu 1:21, 1Timotheo 6:6-7; kumbuka kuwa, hatukuja na kitu chochote duniani hivyo tulivyonavyo sasa
tumepewa na Mungu na tutawajibika kuvitolea hesabu Kwake ya matumizi ya vitu
hivyo tulipokuwa hapa duniani.
· Wajibu wetu ni kumwabudu tu na kumtumikia
Mungu kwa moyo safi na kwa nia njema-hii ndiyo ibada ya kweli.
KUMBUKA: Wote walioonesha moyo wa ibada yaani
kutii na kushuka / kunyenyekea mbele za Mungu walipokea mahitaji yao yote na haja za mioyo
yao.
Kile
unacho kiabudu ndicho kinakuvaa; unakuwa
vile ulivyo kwa kutegemea yule unaye
mwabudu. Zingatia kuwa, ibada ni jumla ya maisha yako; maisha yako ndiyo jumla
ya ibada yako.
Kitu pekee Bwana Yesu anachokitaka na
kukitafuta ndani yetu ni ile roho ya ibada ya kweli au moyo wa utii kwa Neno lake. Hebu angalia
mifano hii michache ifuatayo utaona nini kilitokea pale walipo tii Neno la
Kristo;
§ Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile
akamtokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, mwana wa Daudi; binti
yangu amepagawa sana na pepo. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana,
unisaidie. Akajibu, akisema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia
mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo
mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia mama, imani yako ni kubwa;
na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.
( Mathayo
15:22, 25, 26, 27 na 28. Marko 7:24-30 )
o
Lengo la
Yesu hapa la kumwambia mwanamke huyu kuwa ni mbwa ilikuwa nikutaka kuona kama atakasirika
na kususa kwa kumdhalilisha mbele za watu. Japo kibiblia Mtu asiye mwamini Yesu
ni mbwa, ila ni hatari sana hasa kwa jamii yetu kumwita mwenzako mbwa ; maana
inaweza kuwa vita kali sana. Ila mama huyu haikumsumbua na matokeo yake
akaukumbatia muujiza wake mara. Wengi hukimbia changamoto; kumbe hapohapo ndipo
kwenye majibu yako.
§ Na hapa palikuwa na mtu , ambaye amekuwa
hawezi kwa muda wa miaka thelethini na minane. Yesu alipo mwona huyu amelala,
naye akajua ya kuwa amekuwa katika hali hiyo siku nyingi , akamwambia, Wataka
kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana mimi sina mtu wa kunitia birikani,
maji yanapo tibuliwa, ila ninapokuja mimi , mtu mwingine hushuka mbele yangu.
Yesu akamwambia , simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu
akawa mzima , akajitwika godoro lake , akaenda. Nayo ilikuwa ni siku ya sabato
siku hiyo. Yohana 5:5-9.
o
Kwa
haraka kama binadamu ungejiuliza na kuhoji ; hivi ina maana Yesu kweli, haoni
kabisa na inaonesha hana huruma kwa huyu
mgojnwa kumbebesha godoro na ili hali hajiwezi. Hapa Bwana Yesu alikuwa anataka
kuiona roho ya ibada kwa huyu mgonjwa, kitendo cha yeye tu kutii kauli ya Yesu
ya kubeba godoro kili umba na kufungulia
[ activate ] uponyaji wa kipee kwenye mwili wake na kuinuka mara moja na kuanza
kufanya mambo aliyokuwa hawezi kufanya hapo mwanzo.
§ Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini.
Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya
Siloamu, ( maana yake, Aliyetumwa ). Basi akaenda akanawa; akarudi anaona. Yohana
9:6-7
Katika fungu hilo hapo juu, kitu pekee alichokuwa anakitafuta Yesu kwa huyu kijana kipofu ni ile roho ya
ibada ; utii juu ya kile alichomwambia kufanya. Mara zote miujuza yetu
imeambatanishwa / imefungamanishwa na
utii wetu juu ya Neno la Mungu. Nje ya kulitii
Neno la Mungu tusitarajie kuyaona yale tumwombayo Bwana Yesu ya kitendeka
maishani mwetu. Kwani utii kidogo si utii
kabisa. Tunacho jifunza hapa ni kwamba, kitendo cha kijana huyu kutii
kwenda kunawa bila kuhoji kuwa atakwendaje kwani haoni, kilizaa muujiza wa
kurudi akiona. Haleluya! Haleluya!
§ Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simon,
Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akamjibu
akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi yakuchosha usiku kucha, tusipate kitu;
lakini kwa Neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata
samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika
wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza
vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoyaona hayo,
alianguka magotini pa Yesu, akisema, ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Yesu akamjibu
akamwambia, Simoni, usiogope, tangu sasa utakuwa unavua watu. Luka 5:4-10
· Unaona , hapa kama Petro angekataa kutii neno
la Bwana Yesu, akabaki kujivunia ujuzi wake , nguvu na akili zake na hali
ile ya kushindwa wala asingepata wale samaki. Lakini roho ya utii /
ibada ilizaa muujiza wakutisha wa kupata samaki wengi mno; na jambo la
kushangaza samaki walipatikana katika bahari ileile na eneo lilelile na nyavu
zilezile! Kitu kinacho takiwa ni kuzamisha na kuongeza imani na utii kwa Neno la Yesu. Hata kwako leo inawezekana
kabisa pale tu ukiinua kiwango cha ibada yako mbele za Mungu. Tatizo la watu wengi ni kwamba hutaka Bwana afanye
watakavyo wao na si kama atakavyo Mungu. Hebu tuli tii Neno la Mungu ili lizae
mambo mazuri tuyatamanio maishani mwetu. Maana Neno la Mungu lilikusudiwa
kutiiwa-yaani kulitendea kazi.
”Basi Naamani, jemedari wa jeshi la mfalme wa
Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa
sababu kwa mkono wake BWANA alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu
hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye
ukoma.”
§ Ndipo Naamani aliposikia habari za mtumishi
wa Mungu Nabii Elisha akaenda ili akaombewe na kuponywa ukoma wake. Elisha kwa
uongozi wa Roho wa Mungu akamwambia aende akajichovye mara saba katika mto
Yordani. Lakini Jemedari , Naamani alikataa
pale alipo ambiwa kuwa akajichovye kwenye mto Yordani ; ila baada ya kushauriwa
sana na watumishi wake alikubali akatii agizo la mtumishi wa Mungu , Nabii
Elisha, matokeo alipona na kutakasika ukoma wake kabisa ; hii ni kwa sababu alionesha roho ya ibada ambayo
ni utii.
“Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika
Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake
ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.” 2 Wafalme 5:1, 14
KUMBUKA:
Huwezi kupokea muujiza au majibu ya maombi yako
mpaka tu umeonesha roho au moyo wa ibada; yaani moyo wakushuka chini, heshima na utii mbele za
BWANA YESU.
Mara
zote ukisoma Mwanzo mpaka Ufunuo utaona kuwa, kila aliyemwendea Yesu akitaka
uponyaji au msaada wowote ule kwake, kwanza; Yesu alimpa wajibu wakufanya ikiwa kama sehemu
ya kuangalia moyo wa ibada , yaani kutii .
SURA YA PILI:
AINA ZA IBADA.
Kuna
aina kuu mbili [ 2 ] za ibada, ambazo
ni:-
1. Ibada inayo kubalika mbele za Mungu.
2. Ibada isiyokubalika mbele za Mungu.
1. Ibada
inayo kubalika mbele za Mungu.
Hii ni
aina ya ibada yenye kibali mbele za Mungu, kwani imejikita kwenye misingi bora
ya ibada.
· Misingi mikuu
miwili ya ibada inayokubalika mbele za Mungu
ni:
i. Kumwabudu Mungu katika Roho; Yohana 4:23
ii. Kumwabudu Mungu katika Kweli; Yohana 4:23
I. Kumwabudu Mungu katika roho; Yohana 4:23
§ Hii ni
ibada inayotokea ndani kwenda nje; na siyo kutokea nje kwenda ndani. Ibada hii
haiangalii na wala haiamriwi au kutegemea mazingira fulani; bali shauku ya mwabudu hapa ni huhakikisha amempa
Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yake yote kwani kwake mtu huyu , Mungu
ndiye kipaumbele cha kwanza, na ndipo mambo na mahitaji yake binafsi yanafuata
baadaye. “Bali utafuteni kwanza ufalme
wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mathayo 6:33. Pia katika kitabu
cha Matendo ya Mitume maandiko yanasema;
“Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu
na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine wakiwasikiliza. Ghafula
pakawa na tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisikika, na mara
hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. ” Matendo ya Mitume
16:25-26
vJe,
unafikiri nini kingetokea kama Paulo na Sila
wasinge mfanyia Mungu ibada mle gerezani? Hebu jaribu kuwaza pamoja nami; kuwa,
watumishi hawa wapo kwenye maumivu
makali ya kupigwa na vifungo vya kamba pamoja na njaa kali; lakini mbali na
hayo yote hawakuruhusu mazingira magumu ya gerezani kuwa kikwazo cha kumwabudu Mungu wao; kwani walijua fika
kuwa Mungu wanaye mtumikia na ambaye amekuwa sababu ya wao kupata mateso makali
, peke yake ndiye atakaye waponya pale tu watakapo mpa nafasi ya kwanza hata
kwenye mazingira magumu. Na Mungu hakuwaacha bali alishuka ndani ya gereza na
kuwatoa wote baada ya kuikubali ibada yao.
Kuna
baadhi ya watu kwao ili Mungu awe Mungu kweli ni pale atakapo fanya
wanayoyataka; lakini kumbuka kuwa, Mungu atabaki kuwa Mungu hata kama hakufanya
au kujibu kama ulivyomwomba. Wewe endelea kumwabudu katika Roho na kweli tu
naye atafanya wajibu wake.
§ Ibada
hii inaongozwa na kusimamiwa na Roho
Mtakatifu mwenyewe ndani ya mwamini, ambapo milango mitano ya fahamu haina
nafasi katika ibada hii; mwabudu haongozwi tena na mazingira bali yeye ndiye anayeya
ongoza mazingira . Hapa ndipo roho ya mtu huungana na Roho Mtakatifu kumwabudu
Mungu.
§ Kwa maana Mungu, nimwabuduye katika roho
yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo
kukoma.
o
Warumi
1:9
§ Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Naam, vyote
vilivyomo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu.
o
Zaburi
103:1
§ Dhabihu
za Mungu ni roho iliyovunjika; moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu ,
hutaudharau. Mstari wa 17.
o
Zaburi
51:15-17
vMwabudu
huwa na nia na dhamiri safi ya kumwadhimisha Mungu wake hata kama Mungu
hakufanya kama alivyotaka au alivyo omba.
KUMBUKA: Kama moyo wako hauko sawa , basi
hata ibada yako haitakubalika mbele za Mungu. Na kama tulivyo ona hapo mwanzo
kuwa ibada ni sadaka mbele za Mungu, hivyo basi sadaka yoyote iliyo bora lazima
itoke kwa Mungu mwenyewe.
o
Mfano:
vIsaka
alitoka kwa Mungu; huyu alikuwa ni mwana wa ahadi. Mwanzo 17:15-19 ; 21:1-5
Baada
ya Mungu kumpa Ibrahim , Isaka huyo huyo tena , Mungu akamtaka Ibrahim amtoe
sadaka. Mwanzo 22:1-2, 9-19
vYesu , alitoka kwa Mungu; Isaya 7:14, Mathayo 1:21-23, Yohana 3:16 na
Wafilipi 2:5-11
“Tazama,
bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli;
Yaani, Mungu pamoja nasi.”
Yesu alistahili na kufaa kwani alikuwa ni
mwana wa pekee wa Mungu, lakini pamoja na hayo yote Mungu alimtoa ili awe
sadaka kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu kutoka kwenye utumwa wa dhambi na
makucha ya shetani kisha kumrudishia mwanadamu ufalme / utawala alio upoteza
Adamu pale bustanini Edeni.
Hivyo basi , ibada inayoongozwa na Roho Mtakatifu
itakubalika mbele za Mungu kwani ni sadaka iliyo bora itokayo kwa Mungu
mwenyewe; kwani Roho Mtakatifu ni Mungu
kamili kabisa.
Yohana 4:24
KUMBUKA:
Bila Roho Mtakatifu ni vigumu na wala haitawezekana
kabisa kumwabudu Mungu katika roho na kweli ; bali utakuwa kimwili zaidi.
Hivyo sasa tunamhitaji Roho Mtakatifu ili tuweze kutoa ibada bora na
inayokubalika mbele za Mungu. “Tena
msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi;
bali mjazwe Roho. ..”Waefeso 5:18-21
II. Kumwabudu Mungu katika kweli; Yohana 4:23
Kweli ni visivyo onekana ambavyo kimsingi ni vya milele na milele. Jumla ya kweli yote
ni Mungu na Neno lake.
ü Zaburi
119:142, 160, 2Wakorintho 4:2 , Warumi
1:18- 19, Yohana 18:37-38; 17:17-19. Jumla ya neno lako ni kweli , Na kila hukumu
ya haki yako ni ya milele. Mfano ,
Mungu ni kweli, Yesu ni kweli, Roho Mtakatifu ni kweli, Neno ni Kweli.
ü 2 Yohana
1:2 ; kwa ajili ya hiyo kweli ikaayo
ndani yetu, nayo itakuwa pamoja nasi hata milele.
Hii
sasa ni ibada ambayo misingi yake imejengwa na kukitwa kwenye Neno la Mungu na
siyo hisia na msukumo wa nje.
Angalizo:
§ Usichanganye
Kweli ya Mungu na uongo / uovu. 2Wakorintho 4:2
§ Katika
maisha yako ya ibada hakikisha unabaki katika msingi wa Neno la Mungu ambayo
ndiyo kweli; hata kama milango yako mitano ya fahamu inaonesha au kupingana na
hali halisi bali wewe angalia kweli yaani Neno la Mungu lina sema nini. Hivyo
sasa kama mwabudu halisi hakikisha kuwa umejaa Neno la Kristo kwa wingi. Wakolosai 3:16 ; kwani ujazo wake kwa wingi
ndani yako kutakufanya utoe ibada ya nguvu, iliyo hai na ya kweli baada ya kuwa umelitii na
kuliishi nakukubadilisha tabia, mawazo , nia , hisia,utashi, ufahamu,akili,
elimu, hekima, imani ,na mwenendo wako wa kila siku. Waebrania 4:12 -13
Matokeo
ya ibada inayokubalika:
i.
Mungu
Hutukuzwa. Zaburi 50:23; Atoaye dhabihu za kushukuru,
ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonesha wokovu wa
Mungu.
ii. Waamini Wanasafishwa. Zaburi 24:3-4; Ni nani atakayepanda katika
mlima wa BWANA? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na
mikono safi na moyo mweupe, Asiyeinua nafsi yake kwa ubatili, wala hakuapa kwa
hila.
KUMBUKA:
Ili mwamini afae kumwabudu Mungu lazima maisha yake yawe safi; hivyo tunapaswa
kuishi maisha yatoba na kujitakasa kila
siku ili ibada yetu ipate kibali mbele za Mungu. 2Wakorintho7:1 –tunapaswa kujitakasa nafsi zetu kutokana na
kila kinachotia unajisi mwili na roho huku tukitimiza utakatifu wetu kwa kumcha
Mungu.
iii. Kanisa
linajengwa na kuongezeka.
Matendo
2: 41-47; 5:28; Wakawa
wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega
mkate, na katika kusali. Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu,
wakiumega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa
moyo mweupe. Wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha
kanisa kila siku kwa wale walio kuwa wakiokolewa.
Kwa hiyo, maongezeko na madhihirisho ya
nguvu za Mungu pamoja na ishara na miujiza hutokea pale tu waamini watakapo
inua viwango vyao vya ibada na ushirika kwa waumini wengine na kwa Mungu.
SURA YA
TATU:
JINSI
/ NJIA YA KUMWABUDU MUNGU KATIKA ROHO NA
KWELI.
[
METHOD OF WORSHIP ].
Njia
pekee ya kumwabudu Mungu katika roho na
kweli ni:-
i.
Kujaa
Roho Mtakatifu Na Neno La Mungu;
Ni
kile kitendo cha kuongozwa na Roho Mtakatifu. Ukitawaliwa na Roho na Neno
utaweza kuimba Neno, kuomba Neno, kuongea Neno, kuishi Neno na kulitii Neno
–yaani kulitendea kazi ,kwani maisha yako yamemjaa Mungu.
ü Waefeso 5:18; Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo
mna ufisadi ( matumizi mabaya ya mali isiyo ya kwako uliyo kabidhiwa kuwa
msimamizi-wakili na Mungu ) ; bali mjazwe Roho. Tazama
pia , Warumi 8:14,
ü 1Wakorintho 2:11-12; Maana ni nani katika
binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake?
Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Bali sisi
hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate
kuyajua tuliyo kirimiwa na Mungu.
ii.
Kuelekeza
mawazo yako yote kwa Mungu .
[ Thoughts centered to God ];
Ni ile hali ya kuweka ufahamu wako na akili
zako zote juu ya Mungu. Kumtegemea Mungu kwa kila jambo. Wakolosai 3:2; “yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika
nchi. “
iii. Kutafakari
juu ya Neno la Mungu [ meditating God’s Word ];
Haya ni maisha ya kutenga muda wa kutosha wa
kusoma Neno kwa kujiuliza na kuomba katika Roho. Kama vile mwili unavyo hitaji
lishe bora ili kukua , kustawi na kuimarika hali kadhalika roho ya mwabudu
inahitaji lishe bora ambayo ni Neno la Mungu kila siku. Mathayo 4:4, Yoshua 1:8
ü 2Wakorintho 2:10; Lakini ametufunulia sisi
kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Zaburi
27:4- kuutafakari uzuri wa Mungu siku zote hekaluni mwake. Tazama pia Luka 10:
38-42- kaa chini ya miguu ya Yesu ili umsikilize na kusikia anasema nini juu ya
maisha yako.
KUMBUKA:
Ni katika kutafakari tunapo pata ufunuo
wa Neno la Mungu. Na ili tupate ufunuo safi juu ya Neno la Mungu tunahitaji
kuwa na ushirika wa karibu na Roho Mtakatifu. 2 Wakorintho 13:14, 1Wakorintho
2:10-13.
SURA
YA NNE:
SURA
, PICHA AU MWONEKANO WA IBADA INAYO KUBALIKA.
Sura ni ule mwonekano wa kitu au jambo fulani.
Sura ya ibada inayokubalika kwa Mungu ni manukato au harufu nzuri mbele zake. Kutoka 30:34-38; 37:29, Zaburi 45:8,
Ezekieli 27:22, Yeremia 6:20 na Wimbo ulio bora 4:14
BWANA, akamwambia Musa, Jitwalie manukato
mazuri, yaani natafi, shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato mazuri pamoja
na ubani safi; vitu hivyo vyote viwe ni vya kipimo kimoja.
Yohana 12:3-8; Basi Mariam akatwaa ratli ya
marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu
kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu.
2Wakorintho2:14-16; Ila Mungu ashukuriwe,
anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye
kila
mahali kwa kazi yetu. Kwa maana sisi tu manukato
ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea. Katika hao wa pili harufu ya
mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye
ni nani atoshaye kwa mambo hayo?
KUMBUKA: Ibada inayokubalika huwa kama
manukato mazuri yanayo mfanya Mungu ajisikie vizuri; hivyo humfanya ashuke
ili kutuhudumia watoto Wake. Ili maisha
yetu yawe ya mvuto na harufu nzuri ya kupendeza mbele ya Mungu inatupasa
kujitakasa kila siku maadam tunaishi. 1Yohana
3:3; “Na kila mwenye matumaini haya katika Yeye hujitakasa, kama Yeye alivyo
Mtakatifu. “
Kwa hiyo, Sifa kuu ya Mungu ni Utakatifu /
usafi, kama vile mtu asivyopenda kukaa na mtu mchafu, anayetoa harufu chafu kama
vile kikwapa , miguu, kinywa, n.k hivyo si
zaidi sana kwa Mungu wetu? Yeye ni Mtakatifu hivyo na sisi imetupasa
kuishi maisha Matakatifu yasiyo na michanganyo / ila / mawaa au lawama mbele zake na mbele za wanadamu. 1 P eter 1:16; Maana imeandikwa mtakuwa
watakatifu kwa kuwa Mimi ni Mtakatifu.
Kwa msingi huo, maisha yetu yakiwa safi
chochote tukifanyacho mbele za Mungu kitakuwa ni kama manukato mazuri, hata
unapo omba , maombi yako yatakuwa manukato mazuri mbele ya kiti cha enzi, yaani
Mungu atakuwa anajisikia na kufurahia kwa kile ukifanyacho. Tazama, Ufunuo 5:8; Hata alipo kitwaa kile kitabu,
hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za mwana-kondoo,
kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyo jaa manukato, amabyo
ni maombi ya watakatifu.
SURA YA TANO
SIFA ZA JUMLA ZA MWABUDU.
Mtoa ibada ya kweli au mwabudu halisi [ the
true worshiper ] lazima awe na sifa zifuatazo:-
i. Awe
mtu aliyejaa Imani:
Imani ni
kuishi maisha ya kumtegemea Mungu na Neno lake. Hii humanisha kwamba ,kile alicho
sema Mungu kwenye Neno lake ni lazima aamini kuwa ni kweli na kwamba atafanya
kama alivyo sema. Maana mwenye haki anaishi kwa imani, na pasipo imani haiwezekani
kumpendeza Mungu kwenye maisha yetu. Kama humwamini Mungu hufai kumwabudu. Ni
vigumu kuwaaminisha watu kwa Mungu usiye
mwamini. Wapo watu wanao amini kuwa Mungu anaweza kufanya mambo yote ila siyo
kwao bali kwa wengine. Imani ndiyo mikono ya kupokelea majibu yetu. Matendo
6:5-6, Waebrania11:1,6; Warumi 1:17
ii. Awe
na maisha matakatifu:
1 P
eter 1:16; Maana imeandikwa mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Wakorintho 3:16-17; Hamjui kuwa ninyi
mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho
wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu
atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Mwabudu anapaswa kuwa kioo au kielelezo , maisha yake yawe na ushuhuda mzuri wa
maisha safi yasiyo natuhuma wala lawama. Kwani , Mungu anapendezwa na watakatifu
walioko duniani maana ndiyo walio bora. Zaburi 16:3.
iii. Awe amejaa upendo:
Haya ni maisha ya kutoa na kujitoa kwa ajili Mungu kwanza pili
kujitoa kwa ajili ya wengine. Ukipenda kitu utakifanya kwa moyo wa furaha bila
kuhesabu gharama-yaani bila kutazamia malipo kutoka kwa watu. Ukimpenda Mungu utajitoa
kwa ajili ya kumwabudu na kutumiwa na wengine kwa kadri watakavyo kwani upo kwa
ajili ya kulitumikia kusudi la Mungu. Yohana15:13,
hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya
rafiki zake. Tazama pia , Yohana
3:16, 1Yohana 3:16.
iv. Awe amejaa Neno la Mungu:
Biblia inatusihi sana juu ya kujaa Neno la
Mungu kwa wingi na katika hekima yote, Wakolosai 3:16. Yesu akajibu,
akamwambia, Mtu akinipenda atalishika
Neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao
kwake.
Yohana
14:23. Ukijaa neno , utasema neno, utaimba neno, utaomba neno, utaliishi Neno,
jambo ambalo litakufanya kushinda mazingira yote yakutenda dhambi maishani.
Zaburi 119:9-12.
v. Awe
amejaa Roho Mtakatifu:
Matendo 6:5-6, Stefano alikuwa ni mtu
aliyekuwa amejaa Roho Mtakatifu. Ushirika mzuri na Roho Mtakatifu utakuwezesha
kumfanyia BWANA ibada ya kweli. Ukikosa ushirika na Roho Mtakatifu itakuwa ni
vigumu sana kuwaongoza watu wengine kumtolea Mungu ibada bora yenye kibali kwake.
2Wakorintho 13:14. Kwani hutaweza na
nivigumu kuwapeleka watu mahali wewe
hujafika. Ili watu wakuelewe na wafuate unachokisema ni pale utakapo kiishi
unachokisema. Hakikisha maisha yako yawe yameathiriwa na Roho Mtakatifu.
Waefeso 5:18- tulewe Roho Mtakatifu.
vi. Awe
mtu wa sala / maombi:
Tunaomba
ilikupata msaada wa Mungu katika yale tunayo taka kuyafanya. Lengo kuu la
maombi ni kupata mwongozo sahihi wa Mungu. Vile unataka jambo liwe unaliumba au
unalitengeneza kwenye maombi. Mungu ametuagiza kuomba kwani ndiyo moja ya njia
ya kuwasiliana naye. Anesema katika; Yeremia
33:3; “Niite, nami nitakuitikia nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyo
yajua. “ Pia Zaburi 105:4 ; anasema mtafuteni BWANA pamoja na nguvu zake. Swali
la kujiuliza namwitaje na kumtafutaje Mungu? Jibu ni kwa njia ya maombi/
kuzungumza naye. Hivyo mpendwa fanya maombi ngazi ya kubisha [ maombi ya ngazi
ya patakatifu papatakatifu] ya kuomba katika roho. Mathayo 7:7;
· Kuomba [ ask ]- mwilini ; maombi ngazi ya ua
wa nje.
Maombi
yanayo tawaliwa na milango mitano ya fahamu ,haya ni maombi baridi. Kiwango
hiki hakina matokeo wala madhara kwa adui. Hapa ukiuliza unajibiwa tu. Mfano
unaitwa nani? Amani. Hii haitakusaidia sana.
· Kutafuta [seek ]- nafsi; maombi ngazi ya
patakatifu;
Ni
maombi yanayo tawaliwa na hisia na uzoefu / mazoea , akili na Neno kidogo; ni
maombi ya uvuguvugu. Kiwango hiki cha maombi pia hakina matokeo mazuri na Mungu
hukaa pembeni- utatapikwa na Mungu; mpaka umalize ujanja wote. Hapa mtu
akitafuta atapata anachokitafuta kwa
bidii yake wala Mungu hahusiki na wewe.
· Kubisha [ knock ]-roho; maombi ya ngazi ya
patakatifu papatakatifu;
Ni maombi yanayo tawaliwa na Roho Mtakatifu.
Haya ni maombi ya moto mkali. Kiwango hiki cha maombi ni hatari kwa adui na
wala hawezi kukusogelea na matokeo yake ni makuu sana. Hapa kila anaye bisha
lazima afunguliwe tu; na ukisha funguliwa mlango nikuingia na kujichukulia
unachotaka mbele za Mungu wako. Haya ni maombi ya maarifa na ufahamu wa juu
katika ulimwengu wa roho. Hivyo tunapaswa kuomba siku zote wala tusizimie na
kukata tamaa; Luka 18:1-8
vii. Awe mnyenyekevu:
Mwabudu halisi na wakweli lazima awe mnyenyekevu, kwani anajua wazi kuwa
karama, vipawa na huduma alivyo navyo si
kwa ajili yake ni kwa ajili ya wengine. Na wala siyo vyake amepewa tu bure nay
eye huwa tu ni wakili. Hivyo roho ya kiburi haitatajwa kwake kamwe ; kwani
Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu neema. Ni kweli mtu
akifanya vizuri watu watamsifia lakini wewe usizibinafsishe hizo sifa bali mrudishie
Mungu mwenyewe.
ü 1Petro 5:5-6; Vivyo hivyo ninyi vijana,
watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa
sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi
nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake, tazama
pia ; Yakobo 4:6-7, Mithali 3:34, Ayubu 22:29
KUMBUKA:
Mtu anapo kusifia kwa kufundisha vizuri , kuhubiri vizuri, kuimba vizuri , n.k
jua kuwa kinacho sifiwa siyo wewe bali ni kile kipawa au ile karama na huduma
iliyo ndani yako ambapo kimsingi imetoka kwa Mungu mwenyewe.
vMsingi
Mkuu wa ibada inayokubalika mbele za
Mungu ni USAFI / UTAKATIFU. Katika
Zaburi 24:3-4; maandiko husema, “ Ni nani atakaye panda katika mlima wa BWANA?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu
pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa
ubatili, Wala hakuapa kwa hila.”
Maandalizi ya ibada inayokubalika mbele za
Mungu.
Ni
jambo jema kujiandaa unapo taka kwenda mbele za Mungu. Kuna baadhi ya watu
waliokwenda mbele za Mungu kumfanyia ibada wakiwa wazima wakarudi wakiwa
wagonjwa, wengine walienda wakiwa hai wakarudi maiti. Kwa nini? Kwa sababu Mungu
siyo Mungu wa mazoea ; ni Mungu wa kanuni na taratibu. Walawi 16:1-7
Hivyo,
sasa ni vizuri sana kusafisha mazingira yako yakukutania na Mungu wako kwa
kufanya maombi ya rehema na utakaso mbele za Mungu kwa lengo la kupatana
na Mungu ili tu asione kitu kichafu kisichofaa kwako akageuka na kukuacha; Kumbukumbu la Torati 23:14; Waebrania 4:16; 10:
19-22, Mithali 3:3-4, 1Yohana 3:21 na Yakobo 4:7.
Tazama
pia Yakobo 3:2. “Maana
twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo
ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.” Mungu
anaposhuka anakuja kuhukumu vyote
vilivyo kinyume na ufalme wake. Hivyo ikitokea akakukuta umeharibu na kuchafua
ushirika pamoja naye, atakuharibu. Tazama jinsi Mtume Paulo anavyo likazia
jambo hili katika; 1Wakorintho 3:16-17; “Hamjui
kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na
ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu,
Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo
ninyi.”
Kumbe
saa tunaona kwamba msingi mkuu wa
maandalizi ya ibada yenye maana na kukubalika mbele za Mungu ni mazoezi ya toba, rehema na utakaso katika maisha yetu ya kila siku, yaani usafi wa roho. 1Wathesalonike 5:23; Mungu wa amani mwenyewe
awatakase kabisa; nanyi roho zenu na nafsi zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe
kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
SURA YA SITA
IBADA
ISIYO KUBALIKA MBELE ZA MUNGU.
Ni jambo la kusikitisha, kuogofya na kuumiza
sana; la mtu kwenda mbele za Mungu kumwabudu kisha ibada yake ikakataliwa. Kumbuka kuwa ibada ni sadaka na
kama sadaka basi, ikitokea sadaka yako
imekataliwa hii ina maanisha kwamba na wewe mwenyewe umekataliwa vilevile.
Tazama Mwanzo 4:1-15 utakuta wana wa Adamu, Kaini na Habili walitokeza mbele za BWANA ili
kumfanyia ibada ya kumtolea sadaka. Tunaona sadaka ya mmoja aliye mdogo [
Habili ] ina kubalika na kupata kibali
kwa Mungu ila ya mwingine mkubwa [ Kaini ] haikupata kibali yaani haikukubalika
mbele za Bwana. Mwanzo 4:3-5 inasema
kuwa ; Ikawa hatimaye, Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA.
Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizo nona za
wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali,
wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.
Nini hutokea sasa kwa mwamini kama ibada yake imekataliwa?
Vifuatavyo ni viashiria kuwa mtu huyu ibada
yake mbele za Mungu haina kibali; ni kama anapoteza wakati tu kujihudhurisha
kwenye makusanyiko ya watu wa Mungu. Na kundi hili ndilo kubwa sana. Viashiria
hivi ni:-
I.
Anatawaliwa na roho ya chuki [ hatred spirit
]
II.
ana roho ya wivu [jelous spirit ]
III.
amejaa roho ya kuhukumu na kukosoakosoa wengine
[ judgementalism spirit ]
IV.
ni mtu aliye na roho ya uchungu [ bitterness
spirit ]
V.
anatawaliwa na roho ya kiburi [ eaglism
spirit ]
VI.
mtu wa kujali mipango yake kwanza kuliko
mipango ya ufalme wa Mungu .Kitu ibada, Neno la Mungu kwake ni ziada.
VII.
Mtu mwenye roho ya kutokuonyeka
VIII.
ametawaliwa na roho ya uchoyo na ubahili hata
kwa Mungu.
IX.
amejaa roho ya ubinafsi [ selfishness ]
X.
hujiona kuwa yeye ni bora kuliko wengine.
XI.
anafanya mambo ya Mungu kwa mazoea [ familiar
spirit ]- Waamuzi 16:20-22
XII.
ana roho ya dharau. 1Samweli 2:30
XIII.
ni mwizi / kibaka wa mafungu ya kumi [ robber
] Malaki 3:8-11
XIV.
hana moyo au roho ya shukurani- Mithali 16:18
XV.
amejaa roho ya manung’uniko na lawama. Hesabu
11:4-11; 14:1-12
XVI.
hudharau na haheshimu uongozi na viongozi; haongozeki.
Hesabu 16:1-35 habari za Kora kuinuka kinyume cha Musa; na matokeo yake.
XVII.
huongelea vibaya kanisa lake na watumishi.
XVIII.
hutoa sadaka vilema akidhani anamkomoa
mchungaji. Malaki 1:6-14;
XIX.
ana roho ya kususa kufanya huduma akidhani
ana wakomoa viongozi.
XX.
anaishi maisha machafu yasiyo na ushuhuda mzuri
mbele ya jamii yake-maisha yake humtukanisha Kristo na kuwazuia watu
wasimwamini Bwana Yesu.
XXI.
hana roho ya toba hata kidogo, dhamiri yake imetiwa
ganzi.
XXII.
mtu wakufuatilia na kujihusisha sana na mambo
ya watu kuliko Neno la Mungu.
XXIII.
haongozwi tena na Roho Mtakatifu bali huongozwa
na milango mitano ya fahamu, yaani mwili.
XXIV.
mchongezi, wazushi na mgomvi
XXV.
ana roho ya unafiki [ hypocrisy ]
Kutoka 4:1-15, Malaki 3:8-11;
2:1-4, Zekaria 5:1-4
Mifano ya ibada zisizo kubalika mbele za
Mungu.
Zifuatazo ni baadhi tu ya ibada zisizo
kubalika mbele za Mungu:-
a) Ibada itolewayo kwa miungu [ the worship of
false gods];
miungu ni vitu vinavyo chukua nafasi ya
Mungu. Vitu hivi vyaweza kuwa fedha,
mali, wazazi, kazi na n.k ; hivi ni vitu vya dunia [ earthly materials ] na sanamu za mfano wa vitu vya mbinguni [ heavenly things ]
ambavyo humpelekea mtu kumfanya Mungu
kuwa wa baadaye kabisa. Bwana ni Mungu
mwenye wivu. Kutoka 34:14; “maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa
BWANA, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu. “ Tazama pia- Ayubu 31:24-28, Yoshua
24:19- 20, -ukimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na
kuwatenda mabaya na kuwaangamiza baada yakuwatendea mema. Kumbukumbu la Torati
4:14-19 na Marko 4:19
b)Ibada
itolewayo kwa Mungu wa kweli katika njia au mfumo mbaya.
[ the worship of the true God in a wrong
form.];
Tazama Kutoka 32:1-28, utaona Haruni na wana
wa Israeli wameamua kuyeyusha ndama ili kumwabudu baada ya kuona Musa amekawia
kurudi kutoka mlimani. Mungu hatapokea ibada itolewayo kwake kwa mfumo mbaya;
hapa ni sawa na mtu anaye asi maagizo au neno la Bwana.
c) Ibada
itolewayo kwa Mungu wa kweli kwa namna au kwa mtazamo wa mtu apendavyo yeye. [
the worship of true God in self – styled manners ];
Hii ni roho ya mazoea ya mtu kujiendea hovyo
hovyo au kukosa utaratibu nyumbani mwa Mungu. Usiende mbele za Mungu kwa mazoea ukifikiri
ni Mungu wakumzoelea; usimkariri Mungu, kama jana alitumia kitu fulani basi au
alipitia njia fulani leo anaweza kuja na kitu kingine kabisa. Kama jana alikupa
ufunuo fulani usitumie ufunuo wa jana leo mwamini Mungu kwa kiwango kingine;
usigeuze ufunuo aliokupa jana au mwaka jana na kuufanya fundisho leo , utakuwa
unakosea sana. Jiulize hicho unachokifanya leo umeambiwa na nani au isije ukawa
unakariri na kutembea juu ya mafunuo na shuda za watu; kama unafanya hivyo
utakuwa unawalisha watu viporo na matango mwitu. Hivyo hakikisha kile unacho
kifanya au kukisema, kukiimba na kukifundisha chanzo chake au asili yake iwe ni
Mungu mwenyewe. Leo utashangaa kabisa hata mtoto aliyezaliwa leo kiroho
anashangaa; utakuta watumishi wengi wamegeuza ufunuo kuwa fundisho, elewa kuwa
ufunuo upo ila tatizo kuugeuza ufunuo kuwa fundisho la imani na mtindo wa Mungu kwa watu wake. Mfano
matumizi ya chumvi, maji, mafuta, mchanga, kitambaa, sabuni, udongo n.k,
kwakuwa tu kuna siku ulipewa ufunuo kutumia kitu fulani kwa ajili ya mtu fulani
kwa wakati fulani, sasa mtumishi anageuza kuwa ndiyo mtindo na fundisho la
kuwajenga watu. Huku ni kulinajisi kanisa na kuwadumaza waamini kutokulitegemea
Neno la Mungu ambalo ndilo ufunuo pekee imara na endelevu.
KUMBUKA:
Mungu habadiliki wala Neno lake; bali njia za utendaji kazi wake huweza
kubadilika. Rejea katika huduma ya Yesu wakati wa utumishi wake, alikuwa na njia
mbalimbali za uponyaji: Mfano; siku moja alitema mate na kutengeneza matope
kisha akampaka kipofu machoni na
kumwagiza aende kunawa kwenye birika la siloamu- Yohana 9:1-7, Yesu anaweka
mikono juu ya kipofu Marko 8:22-25, mwanamke anagusa vazi la Yesu na kuponywa ugonjwa wake- Marko 6:56, Akawaagiza wakoma kumi kwenda kujionesha kwa
makuhani ili watakasike na wakiwa njiani wote kumi walitakasika- Luka
17:12…, Akamwamuru aliye pooza miaka 38
kubeba godoro lake mara akawa mzima- Yohana 5:8-9, Yesu analigusa jeneza na kijana aliye kuwa amekufa akawa hai– Luka
7:14, hapa Yesu anamwamuru Lazaro aliyekuwa amekufa kutoka kaburini , mara akatoka akiwa hai- Yohana 11:43, Yesu
analituma Neno tu na kumponya mtumishi wa afisa mmoja - Yohana 4:50, wagonjwa
wanapona kwa kupitiwa na kivuli cha Petro- Matendo 5:15-16, n.k. Acha kumzoelea
Mungu kabisa. Roho ya mazoea ilimgharimu
sana Samsoni, hata ikapelekea kung’olewa macho, kufungwa minyororo, kutupwa
gerezani na kufanyishwa kazi ngumu za kusaga ngano. Waamuzi
16:20-21; Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakuja. Akaamka katika usingizi
wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini
hakujua kuwa BWANA amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho;
wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa
akisaga ngano katika gereza. Kwa hiyo haya ndiyo madhara ya roho ya
mazoea, kung’olewa macho, kuwekwa kifungoni na kutumikishwa kwa kazi ngumu na
adui kama ilivyokuwa kwa kamanda Samsoni. Na katika Matendo ya Mitume 5:1-11;
tunaona habari ya Anania na Safira mkewe waliokufa mbele za BWANA
machoni pa waamini wote kwenye ibada aliyokuwa akihudumu Mtume Petro.
Wanandoa hawa walikufa kwa siku moja baada ya kuongea uongo madhabahuni kwa Mungu.
Waliahidi kuuza kiwanja chao na kwamba wataleta thamani yote ya fedha ya
kiwanja kanisani, lakini baada ya kuuza
wakazuia sehemu ya mali kwa siri; lakini kwa uongozi wa Roho Mtakatifu Petro
akafunuliwa uovu wao. Walipo ulizwa kwa lengo la kutengeneza na Bwana, walizidi kukataa kuwa hicho ndicho kiasi chote
cha pesa. Mara tunaona mzee Anania anapiga mweleka na kufa palepale na vijana
wakaenda kumzika; baada ya masaa matatu mke wa marehemu akaingia na yeye
ibadani kwanza amechelewa sana, pili wamezuia sehemu ya pesa ya Mungu [ wameiba
] na tatu uongo kwani hata alipo ulizwa kuwa kiwanja waliuza kwa pesa ambayo
mme wake aliipeleka; mama huyu bila aibu wala uoga akakubali; hata pale alipo ambiwa mume wako
amekufa kwa uongo huohuo na kuonyeshwa miguu ya vijana waliokwenda kumzika hata
hivyo hakutubu. Ghafla naye akaporomoka chini na kufa palepale na vijana
wakaenda kumzika; huku ibada ikiendelea kama kawaida na Petro akishusha kifungu
kimoja baada ya kingine. Maana yake ni nini; kufa kwako kiroho au hata kimwili kwa uovu
wako usiyotubiwa haitamzuia Mungu kuendelea kuwahudumia watoto wake. Hivyo
angalia sana mapito / njia zako mbele za Mungu, kwani Yeye si wakumzoelea.
Katika Walawi 10:1-20; watoto wa Haruni wanakufa
mbele za BWANA kwa sababu ya mazoea- waliota moto wa kigeni mbele za BWANA
ambao yeye Mungu hakuwaagiza. Akawaua
wote. Pia katika 1Samweli
13:8-14; hapa tunaona mfalme Sauli anaingilia majukumu yasiyo mhusu ya
kikuhani; matokeo yake ufalme wake haukudumu. Usiingilie majukumu yasiyo kuhusu
fanya yaliyo yako. Ijue mipaka ya utumishi wako ili kuepusha ajali nyumbani mwa
Mungu. Ukitazama pia katikati kitabu cha 1Wafalme
13:1-6; utaona kwamba, Mfalme Yeroboamu
alikauka mkono baada ya kufukiza uvumba madhabahuni kinyume cha taratibu.
Katika 2Nyakati
26:16-21; hizi ni habari za mfalme Uzia
aliye acha nafasi yake ya utawala na kuingilia kazi za kuhani za kufukiza
uvumba, makuhani walimkataza lakini alikataa ndipo Mungu alipo amua kumpiga kwa
ukoma kwenye paji la uso mpaka akafa na huo ukoma.
Ukisoma
2Samweli 6:1-9; utaona hapa Uza, anakufa mbele za BWANA kwa kosa la
kulinyoshea mkono sanduku la Agano akitaka kulizuia ili lisianguke.
KUMBUKA : Mungu ni Mungu wa kanuni.
Mathayo 15:1-9; 23:23-28; utaona maisha ya
Mafarisayo na Waandishi yalikuwa ya kinafiki na yakuigiza mbele za Mungu.
Walimheshimu Mungu kwa midomo yao lakini mioyo yao ilikuwa mbali na Mungu. Na
ibada yao ilikuwa bure mbele za Mungu. Pia hata utoaji wao wa zaka, maombi na
sadaka ulikuwa mbaya mbele za Mungu. Walikuwa wanaonekana wasafi nje lakini
ndani wachafu. Tafadhali safisha ndani mwako yaani moyo wako ili ufae kumtolea
Yesu ibada yenye kibali.
d ) Ibada itolewayo kwa Mungu wa kweli katika
Nia mbaya.
[ the true worship of the true God with a
wrong attitude ]
· Nia ni
namna mtu anavyofikiria au mtu anavyohisi au anavyo ona kuhusu mtu mwingine. Nia
ni moja ya vitu vilivyo ndani ya nafsi ya mtu.
ü Warumi 12:2; Wala msiifuatishe namna ya dunia
hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya
Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
Tazama
mfano wa mtu aliye vurugwa nafsi yake hasa chumba cha nia, mara zote maisha
yake ya ibada hayako vizuri ibada au sadaka zake huwa vipofu na kilema mbele za
Mungu. Malaki 1:6-14; mstari wa 8- Tena mtoapo
sadaka aliye kipofu, si vibaya? Na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si
vibaya? Haya! Mtolee liwali wako; je! Atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi
yako? Asema BWANA wa majeshi. Mungu amepiga marufuku kumpelekea matoleo au
sadaka za ubatili.. Isaya 1: 11-20. Mstari wa 13
KUMBUKA:
Kama tukiabudu hali mioyo na hisia zetu haziko sawa au haziko sahihi hiyo ibada
haitakubaliwa na Mungu.
Na
kitu pekee atakacho kifanya Mungu kwa watu wanao abudu kwa nia mbaya, anasema
katika; Malaki 2:3; Angalieni, nitaikemea
mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam, mavi ya sadaka zenu;
nanyi mtaondolewa pamoja nayo. Maana yake hawataziona Baraka za Mungu
katika kile wakifanyacho na pia atawaondolea kibali.
vKiwango
chako cha ibada ndicho kitakacho amua hatima yako; upo vile ulivyo kwa sababu
ya kiwango chako cha ibada mbele za Mungu.
vMatatizo
na changamoto nyingi kwenye maisha ya waamini wengi yanasababishwa na kuwa na
kiwango kidogo cha ibada yaani kukosa roho ya utii juu ya yale tupaswayo
kuyafanya kwa sababu ya roho ya mazoea. Hebu chukulia mfano huu rahisi kabisa
wa wanandoa na mfano wa wazazi na watoto; unafikiri nini kitatokea mke atakapo
mtii mume wake? Bila shaka mume ata mpenda sana mke wake na atatamani awe
anamwona kila wakati. Waefeso 5:22-29, Wakolosai 3:18-19, Mithali 8:17 Mungu
anawapenda wanao mpenda…. Na nini unadhani kitatokea watoto wakiwaheshimu na
kuwatii wazazi wao? Bila shaka chochote kile watoto hawa watakacho kihitaji
kutoka kwa wazazi wao, watafanyiwa. Pia kinyume
chake ikitokea mke hamtii mume wake na wala watoto hawawaheshimu wazazi wao
tena; nina hakika mahusiano katika maisha yao yatakuwa magumu sana. Ndivyo ilivyo katika ufalme wa Mungu kwamaba ili tupate kuyala mema ya nchi inatupasa
kuyatii maagizo ya Neno la Mungu. Tazama, Isaya
1:19-20; Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi. Bali kama mkikataa na
kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya. Usisahau
ibada ni utii.
vPia
nimekuja kungudua kuwa hata vijana wengi wanapata changamoto kubwa katika
mahusiano yao kujua nani ndiye jibu
sahihi kwa ajili yake kutoka kwa BWANA. Utakuta kijana maisha yake ya ibada
niya ujanjaujanja halafu anategemea Mungu ampe mke au mume mwenye busara, kitu
ambacho hakiwezekani kabisa; Mungu anacho kifanya anakuacha upuyange, yaani
ujiendee mwenyewe ukaumie ili ujifunze kutokana na makosa. Kama unataka vya Mungu
lazima vigezo na masharti vizingatiwe; kwani Mungu ni Mungu wa utaratibu.
vTuliokolewa
na kumbolewa kisha tuka hamishwa kutoka kwenye ufalme wa giza na kuingizwa
kwenye ufalme wa nuru ili tuweze kumwabudu na kumtumikia Mungu wetu kwa nguvu
zetu, kwa akili zetu, kwa roho zetu na kwa
mali zetu. Kutoka3:12; 10:24-29.
SURA YA SABA
TOFAUTI KATI YA IBADA NA HUDUMA.
Ipo
tofauti kubwa sana kati ya Ibada [worship ] na Huduma [ ministry ] ; kwa kifupi
ni kwamba:-
· Ibada
kikawaida hutoka chini [ kwetu ] kwenda juu kwa Mungu kwa nguvu za Roho
Mtakatifu kupitia jina la Yesu, ambapo; Huduma ni ile inayotoka juu kwa Mungu
kuja chini [ kwetu ] kwa njia ya Yesu na kwa nguvu za Roho Mtakatifu kwa mfumo
wa karama za rohoni.
ü 1
Wakorintho 12:1-11.
“Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni
yuleyule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni Yeye Yule. Kisha pana
tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni Yule Yule azitendaye kazi zote katika
wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.” 1Wakorintho
12:4-7
KUMBUKA:
Mungu hushushuka kuhudumu kati na ndani yetu na kukutana na mahitaji yetu pale
tu anapokuwa ameipokea ibada yetu, yaani akiwa amefurahishwa na ibada yetu.
v Tatizo
na changamoto kubwa ya kanisa la leo , wakristo wengi tupo kihuduma zaidi na
siyo kiibada; waamini walio kihuduma tunaweza kuwafananisha leo na kizazi cha
Martha ndugu yake na Mariamu, watu wenye shughuli na utumishi mwingi kuliko
kuabudu. Jambo pekee la kujifunza kwa Martha ni kuwa; anawakilisha watu walio
kihuduma zaidi kuliko ibada. Na jambo pekee lakujifunza kwa Mariamu ni kuwa ;
yeye anawakilisha kizazi cha waabuduo halisi ,yaani kundi la waamini walio
jidhabihu au waliyotoa muda, mali na maisha yao kuwa sadaka au ibada iliyo hai
kwa Bwana Yesu. Tazama kile Yesu anachokisema
kwa hawa ndugu pale alipo watembelea nyumbani kwao; kila mmoja alimpa alama
zake:
ü Luka 10:38-42;
Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina
lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye
Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha
alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni
vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie
anisaidie. Bwana akamjibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika
kwa ajili ya vitu vingi; lakini
kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu
amechagua fungu jema, ambalo hataondolewa. Soma pia, Zaburi
27:4; Neno moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalo litafuta, Nikae
nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu niutazame uzuri wa BWANA, Na
kuutafakari hekaluni mwake.
Kwa
hiyo fanya jambo au kitu chochote kitakacho mfanya Mungu ajisikie vizuri na
kushuka kuhudumu, maana sahau kupokea kitu chema kutoka kwa Bwana kama ibada
yako haijamfurahisha. Tangu kale Mungu alikuwa akishuka kuhudumu yaani kuchukua
au kupokea sadaka mara tu yakupendezwa na harufu nzuri ya sadaka au dhabihu hiyo. Mwanzo 4:4-5.
Nikupe
ushauri leo; hebu tafuta kitu ambacho utakifanya katika ufalme wake / nyumbani
mwa Mungu ambacho kitamfanya Mungu huko aliko ajisikie vizuri na kumfanya
achilie majibu ya haja ya moyo wako na kukutendea mambo makuu ya kuushangaza
ulimwengu.
§ Uishi
milele katika uwepo wa BWANA. 2Wakorintho 13:14.
TOLEO LA PILI ( c ) March, 2017.
AMINA
ReplyDelete